WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, (kulia) alipokuwa Mkoa wa Pwani kufunga maonesho ya viwanda mwishoni mwa wiki iliyopita, kushoto ni Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo.
..........................................
Na scolastica Msewa, kibaha
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amempa siku saba Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) linatoa kibali kwa kampuni ya BM Motors cha kutengeneza na
kuunganisha bodi za magari.
Waziri Mkuu alisema hayo wakati akifunga maonesho ya Wiki ya
Viwanda yaliyomalizika mkoa wa Pwani, katika Uwanja wa Sabasaba, Picha ya
Ndege, Kibaha.
Alimtaka Waziri Mwijage, ifikapo Ijumaa wiki ijayo ampe
taarifa ya maendeleo ya kampuni hiyo kuhusiana na kibali hicho kutoka TBS.
Alisema wakati mwingine huo ni urasimu, kama ana tatizo
ambiwe aboreshe hawezi awe amekaa tangu mwaka jana analalamika hajapata kibali
cha kutengeneza mabodi.”
Na kwa nini msimpe hiyo fursa atengeneze bodi halafu mmwambie
arekebishe na mkiwa mmejiridhisha kama ana uwezo wa kutengeneza hayo mabodi na
Watanzania waendelee kutengeneza hapa nchini, badala ya kuagiza nje kwa
gharama kubwa haina maana” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aliongeza kuwa “ulisema unaogopa kutumbuliwa
(Mwijage), sasa sikutumbui nakupa wiki moja nipate taarifa ya mwenendo wa
kampuni yetu ya ndani inayotaka kuunganisha mabasi.”
“Kwanza ni kampuni pekee inayotaka kuunganisha magari
nchini, apewe fursa atujengee magari ya luxury (ya starehe) hapa Tanzania,
alifafanua.
Mapema Waziri Mwijage akisalimia wananchi, alisema kwamba
mashirika yaliyo chini ya wizara yake yakifanya kinyume yanahatarisha ajira
yake, na yeye hayuko tayari kwa hilo.
Waziri Mkuu, aliutaka uongozi wa mkoa wa Pwani kujipanga kwa
kuandaa maonyesho ya viwanda kama hayo kila mwaka, ili wajasiriamali wapate
fursa ya kuonyesha bidhaa zao.
Pia aliagiza miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali
kutumia bidhaa zinazotengenezwa nchini zikiwemo saruji, nondo na mabomba.
Akizungumzia eneo linalomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha
lililopo Kibaha, Pwani, Majaliwa alisema shirika hilo liendelee kutafuta
wawekezaji zaidi kwa eneo hilo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo wakati
akitoa taarifa ya maendeleo ya mkoa huo, alisema shirika hilo
limepata mwekezaji ambapo limetenga eneo la hekta 38.8 kwa ajili ya
ujenzi wa shughuli za kibiashara kama hoteli na maduka makubwa, na hekta
100 ambazo zimetengwa kwa ajili ya makazi.
No comments:
Post a Comment