Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyenyanyua mkono akiwa na Katibu Mkuu
Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel (kulia kwake) wakati wa ufunguzi wa
Mnada wa Kimataifa wa Mifugo Kirumi ulioko wilayani Butiama mkoani Mara.
.............................
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewataka viongozi wote wa
serikali kuanzia ngazi za vijiji,wilaya kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa
rasilimali za mifugo badala ya hali ilivyo sasa ya kuiacha ikitoroshwa kwenda
nchi za nje kwa kuamini kwamba jukumu la ulinzi wa rasilimali hizo ni la Wizara
ya Mifugo na Uvuvi peke yake na ikosesha serikali mapato.
Waziri Mpina ameyasema hayo wakati akizundua mnada wa mpakani wa
Kimataifa wa Mifugo katika eneo la Kirumi Wilayani Butiama mkoani Mara ambapo
ameagiza kufungwa kwa minada yote ya mifugo iliyofunguliwa kinyemela kwani
imekuwa kichocheo cha upotevu wa mapato wa Serikali na kuonya wanaoanzisha
minada hiyo bila kufuata taratibu zilizopo watachukuliwa hatua kali kwa mujibu
wa sheria.
Aidha amemuagiza Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel kuanza
mara kuihakiki minada yote iliyopo nchini ili kuibaini ambayo imeanzishwa
kinyume cha sheria iweze kufutwa.
“wako watu wanafungua minada kila sehemu wanaamua tu wakati taratibu za
ufunguzi wa minada wanazijua kabisa ya kwamba ni lazima wizara iridhie
kufunguliwa kwa mnada huo”alisisitiza Waziri Mpina.
Amesema Serikali inapotaka kuanzisha mnada inakuwa na malengo ya
kuhakikisha biashara ya mifugo inafanyika vizuri na kwamba uanzishaji holela wa
minada unadhoofisha mipango inayowekwa na Serikali jambo ambalo haliwezi
kukubalika.
Naye Katibu Mkuu Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante Ole
Gabriel alisema kufunguliwa kwa mnada huo kutasaidia usimamizi na kudhibiti
utoroshaji wa mifugo na kuongeza mapato ya Serikali ambapo amesema mnada wa
Kirumi umewekwa kimkakati na unatarajia kuvuta wafanyabiashara wa mifugo kutoka
katika nchi za jirani na kuliingizia taifa mapato makubwa.
Waziri Mpina amewataka viongozi wa Serikali kuhakikisha wanapanga
matumizi bora ya ardhi na kuwawezesha wafugaji kupata huduma zinazostahili
ikiwemo malisho na maji badala ya hali ilivyo sasa ambapo kila kiongozi anaona
mifugo ni laana kwa taifa.
Pia Waziri Mpina pia alimuagiza Katibu Mkuu Mifugo kuanzisha haraka ofisi
itayotoa huduma ya vibali kwa watu wanaotaka kusafirisha mifugo nje ya nchi
tofauti na ilivyo sasa ambapo wafanyabishara hao hulazimika kwenda hadi jijini
Mwanza kufuatilia vibali hivyo.
Ameagiza kupelekwa kwa mitungi ya kupandikiza mbegu bora ya mifugo katika
Mkoa wa Mara na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa gharama isiyozidi
sh 5,000 tofauti na ilivyo sasa ambapo hulazimika kugharamia hadi sh, 100,000
kupata huduma hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema Serikali ngazi ya
mkoa huo itaendelea kuwachukulia hatua kali watu wote wataoshiriki vitendo vya
utoroshaji mifugo nje ya nchi huku akiwaonya watu wanaondeleza vitendo vya wizi
wa mifugo kwamba hawatapata tena nafasi katika kipindi hiki cha utawala wa
Serikali ya awamu tano.
Malima alisema tayari mkoa huo umepokea mwekezaji wa kiwanda cha maziwa
kitakachokuwa na uwezo wa kusindikiza tani 200,000 kwa siku na kusema kuwa
itakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wafugaji wa mkoa huo kupata soko la uhakika la
maziwa yao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Mara, Mrida Mshoja amesema
ngombe zilikuwa zinatoroshwa kwenda Kenya na kwamba kufunguliwa kwa mnada huo
kutawezesha wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao na kumshukuru Waziri
Mpina kwa kufanikisha azma ya kuanzisha mnada huo.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akikata utepe kufungua Mnada wa Kimataifa wa
Mifugo Kirumi ulioko wilayani Butiama mkoani Mara juzi, wengine wanaoshuhudia
ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima{kushoto},Mkuu wa Wilaya ya Butiama,
Annarose Nyamubi}kulia} na Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole
Gabriel.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akifunua kitambaa katika jiwe la msingi
la ufunguzi wa Mnada wa Kimataifa wa Mifugo Kirumi ulioko wilayani
Butiama mkoani Mara juzi, wengine wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam
Malima{kulia} na Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel
}kushoto}.
Picha na Story kwa hisani FULL SHANGWE BLOG.
No comments:
Post a Comment