Wednesday, October 17, 2018

DC BAGAMOYO ATAKA WANAFUNZI KIDATO CHA NNE KUJIANDAA NA MTIHANI.

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Zaynabu Kawawa. 
...........................

Na Omary Mngindo, Lugoba

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Zaynabu Kawawa, amewataka wanafunzi wa sekondari ya Lugoba kujiandaa vyema na mithihani yao ya kidato cha nne, inayotaraji kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao.

Kawawa ameyasema hayo katika mahafari ya 27 shuleni hapo ambapo alisema maandalizi mazuri kwa ajili ya mitihani ndiyo itayowawezesha kufanya vyema, hatimae kufikia malengo waliyojiwekea, huku akiwataka wazazi kuchangia sekta hiyo ili kukabili changamoto zilizopo. 

Mkuu huyo aliongeza kwamba serikali inaendelea na uboreshaji wa sekta ya elimu sanjali na kuongeza walimu, kukarabati miundombinu hiyo ikiwemo utoaji wa fedha kila mwezi kutoka serikalini.

"Serikali inataka kuboresha zaidi elimu kuanzia ya msingi na sekondari, ili iwe sawa na ya wanafunzi wasio na ulemavu, hatua inayolenga kuwepo elimu jumuishi kwa wanafunzi wote pasipokubagua," alisema Kawawa.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha sekta hiyo ikiwemo wanafunzi wenye ulemavu, huku akipongeza wadau waliojenga darasa la wanafunzi wa elimu maalumu hali inayopaswa kuungwa mkono.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Abdalah Sakasa alimwambia Mkuu hiyo kuwa changamoto inayowakabili ni pamoja na gharama ya kununulia kemikali na vifaa vya maabara kipindi cha mitihani ya kitaifa.

Alisema kuwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1989 ikiwa ni shule za mwanzoni kwa sasa ina idadi ya wanafunzi wapatao 1,388, ambapi kati ya hao wanafunzi waliohitimu wakiwa 73 ambao ndio walioagwa kwenye mahafali hayo.

"Kwanza tunaishukuru serikali iliyoko madarakani chini ya rais Dkt. John Magufuli kwa kuendelea na utoaji wa fedha kwa ajili hiyo, lakini hazikidhi kutokana na gharama kuwa kubwa, tunaiomba kuangalia uwezekano wa kutuongezea ili kuongeza ufanisi wa masomo ya Sayasi", alisema Sakasa.

Aliongeza kwa kusema kwamva changamoto hiyo imekuwa kubwa, hasa ikizingatiwa kwamba shule hiyo ina wanafunzi wengi wanaosoma masomo ya Sayansi.

"Mbali ya changamoto hiyo, pia tunakabiliwa na uchakavu wa sakafu katika baadhi ya madarasa, utatuzi wake ni kuweka marumaru, kuuna madarasa 17 kila darasa moja linagharimu shilingi milioni mbili,"alimalizia Sakasa.
 
Hawa ni baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Lugoba

No comments:

Post a Comment