Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Mfaume Kawawa katika kikao na wawekezai na wafanayabiashara Bagamoyo.
......................
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Mfaume Kawawa
amewataka watumishi wa serikali wilayani humo kuacha kufanya kazi kwa mazoea na
badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia Kanuni, Maadili na kujituma zaidi
katika kuiletea wilaya maendeleo na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni alipokuwa
akizungumza kwenye kikao kilichowajumuisha wadau wa maendeleo wilayani Bagamoyo
wakiwemo wawekezaji wenye viwanda, wafanya biashara, pamoja na wakuu wa idara
lengo likiwa ni kuangalia ni mambo gani yanayokwamisha kufikia malengo kwa
wawekezaji na wafanya biashara ndani ya wilaya hiyo.
Alisema Maendeleo hayapatikani kama hakuna
ushirikiano kati ya watendaji wa serikali na wawekezaji au wafanyabiashara ambao
uwepo wao unasaidia ajira kwa wananchi, na kulipa kodi itakayofanya maendeleo
yenye manufaa kwenye jamii.
Kawawa alisema hataki kuona mtendaji wa serikali
anafanya kazi kwa mazoea kwa kudharau watu wanaohitaji msaada wake katika
kufanikisha jambo na kuonya kuwa mtunishi atakaebainika kukwamisha maendeleo
Bagamoyo atamchukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia vivutio vilivyopo Bagamoyo ambavyo
vinaweza kuingizia wilaya mapato kwa wageni, aliwataka watendaji wa idara ya
mambo ya kale kubuni mbinu zitakazowavutia watalii wa ndani na nje ya nchi kufika
Bagamoyo kujionea mambo mbalimbali ya kihistoria ili serikali nayo iongeze
mapato.
Alisema si vyema kuweka sheria kandamizi kwa
watalii kwani kufanya hivyo kutapelekea kupunguza watalii na kupunguza mapato
ya serikali yanayotokana na watalii.
Awali wakichangia mada katika mkutano huo,
wawekezaji na wafanyabiashara wametaja changamoto mbalimbali zinazowakwamisha
kufikia malengo yao ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa maji ya uhakika na umeme
wa uhakika hali inayopelekea kuzorota kwa uzalishaji huku wengine wakishindwa
kabisa kuanza uzalishaji.
Kwa upande wao wafanyabiashara wamelalamikia kodi
zinazokadiriwa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kuwa hayazingatii uhalisia wa
biashara husika hivyo hukadiriwa kodi kubwa inayopelekea wafanyabiashara
kushindwa kulipa na hatimae kufunga biashara.
Walisema ni vyema makadirio ya kodi yakafanywa
kwa uhalisia wa biashara husika ili watu wengi waweze kuendesha biashara na
kulipa kodi kuliko ilivyo sasa biashara nyingi zimefungwa kwasababu ya madeni
makubwa yasiyolipika.
Kufuatia malalamiko hayo wakuu wa vitengo vya
DAWASA, TANESCO na TRA wamepata nafasi ya kujibu hoja zilizowasilishwa ambapo Meneja wa DAWASA Bagamoyo alisema katika
kuhakikisha tatizo la maji linaondoka katika wilaya ya Bagamoyo DAWASA inaendelea na mradi wa ujenzi
wa tenki la kuhifadhi na kusambaza maji katika maeneo ya mji wa Bagamoyo lenye
ukubwa wa mita za ujazo 6000, ambalo lina uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni
sita.
Alisema
Tenki hilo litakapokamilika litahudumia wananchi wa maeneo ya Mpiji, Zinga,
Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya, Bagamoyo mjini na ukanda maalum
wa ewekezaji EPZA.
Nae
Meneja wa TANESCO wilaya ya Bagamoyo Daniel Kyando alisema kutokana na
miundombinu iliyopo TANESCO Bagamoyo ina uwezo wa kuhudumia megawatts 22 ambapo
mpaka sasa Bagamoyo umeme unaotumika ni megawatts 9 tu.
Akizungumzia
swala la kukatika kwa umeme katika mji wa Bagamoyo, kyando alisema hiyo
inatokana na matengenezo yanayofanywa na mafundi katika kuimarisha miundombinu
hasa katika kipindi cha mvua.
Kwa
upande wake Meneja wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA) wilaya ya Bagamoyo,
Farence Mniko alisema TRA Bagamoyo inaendele kushirikiana na wafanyabiashara
ili kuhakikisha kila mmoja analipa kodi inayomstahiki.
Akizungumzia
swala la wafanyabiashara wenye madeni makubwa na kupelekea kufunga biashara
zao, Meneja Mniko aliwataka wafanyabiashara hao kufika ofisi za TRA ili kuona
namna bora ya kulipa madeni hayo au kusamehewa ikiwa watakidhi vigezo vya
kusamehewa baada ya kujaza fomu ya msamaha.
Meneja wa TANESCO wilaya ya Bagamoyo Daniel Kyandoakizungumza katika mkutano huo.
Meneja wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA) wilaya ya Bagamoyo, Farence Mniko akizungumza katika mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Mfaume Kawawa (katikati) akiwasikiliza wawekezai na wafanayabiashara Bagamoyo katika kikao alichokiitisha hivi karibuni katika Hoteli ya Green Park.
Wawekezai, wafanayabiashara na wakuu wa idara wilayani Bagamoyo, wakiwa katika kikao cha pamoja alichokiitisha Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa.
No comments:
Post a Comment