Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunawashikilia watu wawili wanaofahamika
kwa majina ya Mgassa Carlos @ Jeremiah, miaka 42, mkazi wa Bulele na Jafari
Swalehe, miaka 57, kwa kosa la kumtorosha kusikojulikana mtuhumiwa aitwaye
Hasan Bushangama, @ Ngalinda, miaka 43, katibu Mwenezi wa CCM kata ya Buhongwa,
aliyekuwa amekamatwa na Polisi kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha
pili jina tunalihifadhi, mwenye umri wa miaka 17, shule ya sekondari buhongwa,
baada ya kumchukulia mdhamana Polisi, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Tukio hilo la kumpa mimba mwanafunzi liliripotiwa kituo cha Polisi miezi
miwili iliyopita ambapo baada ya kuripotiwa polisi tulifanya msako mkali na
kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa. Aidhaa wakati tukiendelea kumshikilia
mtuhumiwa kituoni kwa mahojiano zaidi, watuhumiwa wawili tajwa hapo juu
walifika kituoni kumchukulia mdhamana huku wakiwa wamekamilisha taratibu zote
kisheria. Pia kwasababu ni haki yake kisheria mtuhumiwa kupewa dhamana
kulingana na kosa analotuhumiwa nalo basi polisi tulimpatia dhamana.
Ndipo wakati polisi tulipomhitaji mtuhumiwa kituoni ili tuweze
kukamilisha taratibu za kumfikisha mahakamni hakufika na alipotafutwa
hakupatikana na baadae tulipata taarifa kuwa ametoroka. Baada ya kupata
taarifa hizo tulifanya msako mkali wa kuwakamata wadhamini wake wote wawili na
kufanikiwa kuwakamata na tayari tumewafikisha mahakamani.
Katika tukio la pili; Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunamtafuta mtu
mmoja aliyefahamika kwa jina la Zephilin Michael, miaka 43, katibu mwenezi wa
CCM kata ya Mkolani, maarufu muuza kahawa, kwa tuhuma za kumlawiti kijana mmoja
jina tunamhifadhi huko kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo AMani iliyopo
Mtaa wa Mkolani Wilayani Nyamagana , kitendo ambacho ni kosa la Jinai.
Tukio hilo limetokea tarehe 26.10.2018 majira ya saa 11:30hrs, hii ni
baada ya mtuhumiwa kumuajiri kijana huyo kwenye kazi ya kuuza kahawa mtaani
kisha alimpangishia chumba namba tatu katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Amani
ili pindi anapotoka kuuza kahawa awe anafikia hapo. Ndipo tarehe na majira
tajwa hapo juu mtuhumiwa alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni na
kumuuliza mhudumu kama kijana wake yumo ndani ya chumba chake ndipo alielezwa
na mhudumu yupo ndani na yeye alimfuata humo chumbani huku mhudumu akiendelea
na shughuli zake.
Aidha baada ya muda mchache kupita ilisikika sauti ya mtu akipiga kelele
toka ndani ya chumba hicho na baadae watu walipochungulia kupitia dirishani
walimuona mtuhumiwa akimlawiti kijana huyo. Ndipo walipomtaka afungue mlango
aligoma na baadae alifungua na kutoroka na kijana huyo pia alitoroka kisha
wananchi walitoa taarifa polisi. Polisi tunaendelea na msako mkali wa
kuwatafuta watuhumiwa wote wawili ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa wakazi wa jiji na Mkoa
wa Mwanza tukiwataka waache tabia hizo mbaya za ubakaji na ulawiti kwani
ni kosa kisheria na endapo mtu yeyote atabainika hatua stahiki za kisheria
zitachukuliwa dhidi yake. Vilevile tunawaomba wananchi waendelee kutoa
ushirikianao kwa Jeshi la Polisi kwa kutupa taarifa za uhalifu na waalifu ili
waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment