Thursday, October 18, 2018

SUBIRA MGALU ATOA MSAADA WA TAA ZA KISASA KATIKA ZAHANATI ILI KUKABILIANA NA TATIZO LA UKOSEFU WA UMEME

MBUNGE wa viti maalum Mkoani Pwani, Subira.

NA MWAMVUA MWINYI,PWANI

MBUNGE wa viti maalum Mkoani Pwani, Subira Mgalu ,ametoa msaada wa taa za kisasa, zinazotumia umeme wa jua katika zahanati zaidi ya hamsini ,kati ya 121 ambazo zinatoa huduma ya kuzalisha akinamama Mkoani humo .
Lengo la kusambaza taa hizo ni kupunguza changamoto ya ukosefu wa umeme wa uhakika katika zahanati hizo .

Akielezea juhudi hizo alizozichukua ,wakati akizungumza na wananchi wa Ngolongo na Mloka ,wilayani Rufiji ,Subira alisema alifanya tathmini na tafiti na kubaini zipo zahanati 121 mkoa mzima ambazo zinatumia solar ama hakuna umeme kabisa .

Alieleza kufuatia tathmini hiyo ,alifanya jitihada za kupata taa hizo ,zenye uwezo wa kuongeza umeme kwenye simu ,kuwasha tochi na taa ili kusaidia kuboresha huduma ya afya.

“Kwa sasa nimeshazifikia zahanati karibia 50 na natarajia kuzimaliza zahanati 121 ,kwa kuzipatia taa mbili mbili kila zahanati ifikapo mwishoni mwa mwezi huu” alifafanua .

Akijibu malalamiko ya wananchi kuhusu kutofikiwa na umeme ,mbunge huyo ambae pia ni naibu waziri wa nishati alilitaka ,shirika la umeme (Tanesco ) kwamba umeme usiishie barabarani ufike kwa wananchi .

“Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa hydro power (stigo) wilayani hapa ,hivyo nawahakikishia wananchi vipo vijiji vimetajwa kufikishiwa umeme kupitia mradi huu”

“Vijiji vitapata umeme kila mtaa ikiwemo Ngolongo Mashariki ,Ngolongo Magharibi ,Kilimani Mashariki ,Kilimani Magharibi ,Mloka, Nyamwinyili,Ndundunikanza,Msona,Kipugila ambavyo vimetajwa kwenye andiko la mradi kitaifa na kimataifa ,” alifafanua Subira .

Alieleza, lakini wale wenye mahitaji ya umeme wa haraka Tanesco iwaunganishie na kuwawekea nguzo na wengine wasubiri umeme wakati mradi ukitekelezwa.

Awali baadhi ya wakazi akiwemo Issa Kabandika alisema ,umeme ukifika Mloka utakuwa kichocheo cha maendeleo yao lakini bado haujafika mitaani kwani nguzo zipo barabara kuu .

Sultan Mbena na Hiyari Puga walimshukuru Rais Dk.John Magufuli na serikali kwa hatua ya mradi huo wa stigo ,na wanaomba uendelee kwa maslahi yao na nchi 

No comments:

Post a Comment