MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri.
NA TIGANYA VINCENT,RS TABORA.
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amewaagiza
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kuhakikisha hakuna mtoto anayeanza Darasa la
Kwanza bila kuwa amepitia darasa la Awali.
Hatua hiyo inalenga kuondoa tatizo la kuwa na
wanafunzi wanaoingia Darasa la Kwanza ambao hawajui kusoma, kuhesabu na
kuandika.
Mwanri alitoa kauli hiyo hivi wakati akifungua mkutano wa kutathmini masuala
ya elimu mkoani humo na kuhimiza walimu kuhakikisha wanaondoka tatizo la KKK
shuleni kwao.
“Msingi mzuri wa mtoto lazima uanzie elimu ya awali na ndio maana
nasistiza kuwa mtoto asiingie la kwanza kama akupitia Chekechea …kule ndipo
mtoto anapoandaliwa kuwa na maendeleo mazuri kitaaluma …ukikosea toka hapo basi
mtoto anaweza kutokuwa na maendeleo mazuri darasani” alisema.
Alisema vitendo vya baadhi ya walimu kutozingatia hilo na kuchukua watoto
ambao hawakupita elimu za awali ndiko kunakosababisha baadhi yao wanapofanya
mitihani ya kujipama ya Darasa la Nne matokeo yao sio mazuri kwa sababu ya
kuanza la kwanza hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Aidha Mwanri aliwapongeza walimu wa Shule za Awali na msingi kwa kazi
kubwa wanayofanya ya kuwatengenezaea msingi mzuri watoto hao ili wanapoendelea
na masomo yao waweze kufanya vizuri.
Katika hatua nyingine amewataka wamiliki na walimu wa Shule za Awali
kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri kwa watoto hao ili wapende kwenda shule.
Alisema maeneo hayo lazima yawe na vivutio wa michezo mbalimbali ya
watoto wadogo ili pamoja na kujifunza wawe na muda wa kucheza kama sehemu ya
burudani na elimu kwao.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora ametoa wito kwa wazazi na
wadau wengine kuweka mazingira mazuri ambayo yatawavutia walimu hasa wale
ajira mpya kupenda kufanya kazi katika maeneo yao.
Alisema mazingira hayo ni pamoja na kuwawekea vivutio kama vile kuwapa
maeneo ya kulima , nyumba za kuishi kama hakuna nyumba za shule na wakati
mwingine kuwapa chakula cha kuanzia maisha.
Mwanri alisema kuna baadhi ya maeneo hapa nchini yamefanikiwa kielimu
kutokana na wazazi kuweka vivutio ambavyo vimewafanya walimu wanaporipoti
kutofikia kuhama katika shule walizopangiwa.
“Tujenge utamaduni wa kuweka motisha kwa walimu wetu…kwa mfano mnaposikia
leo kuna mwalimu mpya anaripoti katika shule yetu , mnaweza kukusanyika na
kumlaki ili ajiene kuwa amefika nyumbani na sio ugenini” alisema.
No comments:
Post a Comment