Tuesday, October 23, 2018

KAMPUNI YA SAYONA YAKABIDHI VIFAATIBA VYA SHILINGI MILIONI TANO CHALINZE.


Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sayona,Bw Aboubakary Mlawa kulia akikabidhi vifaa hivyo kwa Diwani wa kata ya Talawanda.
....................................
 
Kampuni ya Sayona Fruits Limited ya Mboga Chalinze imekipatia Kijiji cha Magulumatali vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni Tano  kwa ajili ya Zahanati ya kijiji hicho.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Diwani wa kata ya Talawanda, Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sayona,Bw Aboubakary Mlawa alisema msada huo unatokana na uhitaji wa huduma ya afya katika kijiji hicho.

Alisema baada ya kupata taarifa ya kumalizika kwa ujenzi wa zahanati hiyo ambao ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na wananchi alitembelea kijijini hapo na kukuta changamoto ya vifaa na hivyo kampuni yake kuamua kuwasaidia.

Bw Mlawa alisema vifaa hivyo vitasaidia sasa kuanza kwa huduma katoka zahanati hiyo ambayo ilishindwa kutoa huduma kutokana na kutokuwepo kwa vifaa .

Naye Diwani wa kata hiyo Bw Said Zikatimu akishukuru kwa niaba ya wananchi alisema licha ya kukamilika kwa ujenzi zahanati hiyo ilishindwa kuanza kutoa huduma kutokana na kukosekana kwa vifaa tiba.

Alisema Halmashauri iliwapangia Madaktari na wahudumu katika zahanati hiyo lakini hawakuweza kutoa huduma kutokana na kusubiri mchakato wa ununuzi wa vifaa.

"Kwa kweli tunawashukuru Sayona kwani sasa huduma zitaanza  kwa vifaa hivi lakini pia Halmashauri itaendelea na mchakato wake wa kuleta madawa"alisema Diwani huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Hlamaahauri ya Chalinze.

Vifaa vilivyotolewa na Sayona Fruit Limited Mboga ni pamoja na vifaa vya huduma kwa wagonjwa mchanganyiko sambamba na vifaa vya uzazi na huduma kwa watoto. 

Sayona imekuwa ikisaidia sekta mbalimbali katika huduma za jamii,sambamba na kuwasomesha watoto ambao wazazi wao hawana uwezo katika elimu ya sekondari katika Halmashauri ya Chalinze.
 

 Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sayona,Bw Aboubakary Mlawa kulia, akimkabidhi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Saidi Zikatimu vifaa hivyo.

No comments:

Post a Comment