Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
akisisitiza jambo mbele ya Wabunge wa kamati ya Huduma za Jamii na Wadau wa
Masuala ya Afya (hawapo kwenye picha) katika uzinduzi wa taarifa ya utafiti wa
Viashiria vya Malaria nchini.
.......................................
Na WAMJW – Dar Es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu amewaagiza Maafisa Afya nchini kusimamia kwa ukamilifu usafi wa
mazingira katika jamii ili kutokomeza ugonjwa wa Malaria.
Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo Oktoba 22, 2018 wakati akizindua
Taarifa ya Utafiti wa Viashiria vya Ugonjwa wa Malaria wa Mwaka 2017 katika
Ukumbi wa Karimjee jijini Dar Es Salaam.
“Nawaagiza Maafisa Afya, badala ya kupoteza muda mwingi wa kukagua
migahawa, bucha za nyama na sehemu ambazo wanajua zinaleta fedha, tunataka pia
wajikite katika kusimamia usafi wa mazingira katika Kata, Vijiji na Mitaa
yetu”Alisema Mhe. Ummy.
Katika kuhakikisha hali ya usafi wa mazingira inakuwa endelevu, Waziri
Ummy ameagiza Mabalaza yote ya Halmashauri nchini kuweka Sheria na adhabu kali
kwa wote ambao wamekuwa wagumu katika kushiriki katika usafi wa mazingira huku
Waganga Wakuu wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia vyema
utekelezaji wa kanuni na sheria za afya na usafi wa mazingira jambo ambalo
litaibua chachu ya ushindi katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria.
“Niyatake Mabalaza ya Hamashauri kuweka hatua kali, sheria kali na adhabu
kali kwa wote ambao hawashiriki katika usafi wa mazingira” alisema Waziri Ummy.
Licha ya hivyo Waziri Ummy alisema kuwa Serikali kupitia Wizara
inaendelea kutekeleza Mpango endelevu wa ugawaji vya ndarua kupitia wanafunzi
wa shule za msingi, kupitia Kliniki za wajawazito na watoto, ambayo hujulikana
kama Chandarua Kliniki huku hadi sasa jumla ya vyandarua milioni 31 vimeshagawiwa
nchini kote.
Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa Matokeo ya mpango endele u wa ugawaji wa
vyandarua yameonesha kuwa asilimia 78 ya kaya nchini Tanzania zinamiliki
angalau chandarua kimoja chenye dawa, Katika utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto
na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2015-16, ni asilimia 66 tu za kaya zilikuwa
zinamiliki angalau chandarua kimoja chenye dawa huku Umiliki wa vyandarua
vyenye dawa ni wa kiwango cha juu kwa kaya za mijini (asilimia 81)
ikilinganishwa na kaya za vijijini (asilimia 77).
Kwa upande mwingine Waziri Ummy alitaja Halmashauri zenye maambukizi ya
kiwango cha juu ni pamoja na Kakonko 30.8%, Kasulu DC 27.6%, Kibondo DC 25.8%,
Uvinza 25.4%, Kigoma DC 25.1%, Buhigwe 24%, Geita DC 22.4%, Nanyamba TC 19.5%,
Muleba DC 19.4%, Mtwara DC 19.1%, huku Halmashauri zenye maambukizi ya
kiwango cha chini ya asilimia 0.1 ni Mbulu TC, Mbulu DC, Hanang, Hai, Siha,
Moshi MC, Mwanga, Kondoa TC, Meru DC, Arusha CC, Arusha DC, Munduli,
Ngorongoro, Rombo DC
Mkurugenzi
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akionesha Kitabu cha Taarifa ya
utafiti wa Viashiria vya Malaria mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa
uzinduzi wa taarifa ya utafiti wa Viashiria vya Malaria nchini uliofanyika leo
jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikata
utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa taarifa ya utafiti wa Viashiria vya Malaria
nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
wakioneshana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya TAKWIMU Dkt. Albina
Chuwa (wakatikati).
Wabunge
wa Kamati ya Huduma za Jamii na Wadau wa Masuala ya Afya wakifuatilia taarifa
ya Utafiti ya Viashiria vya ugonjwa wa Malaria nchini iliyokuwa ikisomwa na
Mgeni rasmi Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye Picha) jijini Dar
es salaam.
No comments:
Post a Comment