Mkurugenzi
wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi
.................................................
Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, CHINA.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Hassan Abbasi ametunukiwa cheti cha Uprofesa wa Muda (Part Time and Research
Professor) katika Kitivo cha Lugha na Utamaduni wa Kigeni katika Chuo Kikuu cha
Mawasiliano na Habari cha China (China Communication University).
Tuzo hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitivo hicho kwa kutambua mchango wa Dkt.
Abbasi katika tasnia ya habari, utafiti na lugha ya Kiswahili.
Akizungumza wakati wa hotuba yake chuoni hapo kuhusu hali ya sekta ya
habari nchini Tanzania, Dkt. Abbasi amesema kuwa vyombo vya habari vina wajibu
wa kusaidia maendeleo ya nchi na kuwa chachu ya amani na si vurugu.
“Sisi kama wanahabari au vyombo vya habari tunapaswa kuwa na weledi na
wajibu wetu mkuu ni kusaidia maendeleo ya nchi na si kuzigawa jamii au
kuzitofautisha. Waandishi wa habari wa hapa China ni mfano mzuri wa kile
ninachokiita uandishi wa habari za kimaendeleo na si za kimapokeo ” amefafanua
Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi ameshauri vyombo vya habari nchini Tanzania kutobaki
na mfumo mmoja wa utoaji taarifa bali kujiimarisha katika mifumo mingine ya
kidigitali kwani dunia imehama kutoka analojia kwenda digitali.
Hata hivyo, kabla ya kuhutubia wanafunzi wa kitivo cha utamaduni na lugha
za kigeni chuoni hapo, Dkt. Abbasi alipata fusra ya kuzungumza na Naibu Mkuu wa
Chuo Prof. Zhang Shu Ting na kuahidiana kushirikiana katika mambo mbalimbali
yanayohusu sekta ya habari na mawasiliano.
“Urafiki kati ya China na Tanzania utadumu daima, kutokana na faida
tunazozipata kati yetu sisi tutafanya kila jitihada kushirikiana nanyi”
ameongeza Dkt. Ting.
Jumla ya Watanzania 22 wameshamaliza masomo yao katika chuo hicho pekee
kinachotoa masomo yake kwa lugha ya Kiingereza nchini China ambapo hadi sasa
Watanzania wanaoendelea na masomo ni 7.
Chuo cha Mawasiliano cha China kilianzisha mwaka 1964 na ni moja ya vyuo
vya kimataifa vinavyotoa masomo ya habari na mawasiliano.
Katika ziara hiyo, Dkt. Abbasi ameambatana na Wakuu wa Vitengo vya
Mawasiliano kutoka taasisi mbalimbali za umma nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment