Thursday, October 18, 2018

MWAMBISI SEKONDARI KIBAHA WALILIA UMEME

Na Omary Mngindo, Kongowe

SHULE ya sekondari ya Mwambisi Forest iliyoko Kata ya Kongowe Kibaha Mji Mkoa wa Pwani, haina huduma ya umeme kwa kipindi cha miaka sita sasa, tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.

Shule hiyo ambayo inapakana na Hifadhi ya Msitu wa Kongowe mjini hapa (Kongowe Forest) ipo umbali wa mita 100, ambao ni sawa na urefu wa nguzo mbili za umeme ili ufike shuleni hapo.

Hayo yamebainika katika taarifa ya Wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo, iliyosomwa na wanafunzi Leah Samson na Fahad Salimu mbele ya mgeni rasmi Nabii Jofrey, Mwalimu Mkuu Josefu Simba na diwani wa Kata hiyo Idd Kanyalu.

Imeeleza kuwa kukosekana kwa nishati hiyo kunachangia kushindwa kutumika baadhi ya vifaa ambavyo vingesaidia kuboresha taaluma, pia ulinzi wa mali zilizopo shuleni hapo, na kwamba ulipoishia umeme kuna umbali wa mita 100 sawa na nguzo mbili.

"Mbali ya ukosefu wa umeme, changamoto nyingine ni uhaba wa vyumba vya madarasa, viti, meza, jengo la Utawala, ongezeko la wanafunzi, upingufu wa vifaa vya kujifunzia, uzio na idadi ndogo ya walimu wa somo la Baiolojia," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumza na wahitimu hao, Nabii Jofrey alisema kuwa amepokea changamoto hizo, huku baadhi yake akazitolea majibu hapahapo nyingine akiahidi kuzibeba kwa lengo la kwenda kuzitafutia ufumbuzi.

"Nitatengeneza meza 18 za walimu, nitanunua vitabu nitavyoelekezwa vya kiada pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kufundishia," alisema Nabii Josefu.

Awali mwalimu Simba alisema kwamba shule hiyo pamoja na kuwa ya mfano katika utunzaji wa mazingira, wanaushukuru uongozi wa Hifadhi ya Misitu Kongowe kwa kuwapatia miti na wataalamu wa kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Diwani Kanyalu alianza kwa kumshukuru mgeni rasmi kwa kukubali mwaliko huo, huku akieleza kwamba anaimani kubwa kwamba changamoto alizoziahidi atazitekeleza mapema iwezekanavyo.

No comments:

Post a Comment