Friday, October 19, 2018

WAZIRI MWIJAGE AZINDUA KIWANDA CHA VILAINISHI KIGAMBONI.



 Waziri wa Viwanda,  Biashara na Uwekezaji,  Charles Mwijage akifungua kitambaa ikiwa ni ishara ya kuzindua Kiwanda cha vilainishi katika wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Na Selemani Beta

Waziri wa Viwanda,  Biashara na Uwekezaji,  Charles Mwijage amezitaka Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). kuliangalia kwa jicho la karibu soko la vilainishi hapa Nchini kwani hivi sasa soko hilo limekuwa na bidhaa ambazo hazikidhi ubora unaokubalika.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda kipya cha vilainishi cha Lakes Lubes, kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mwijage alisema kwa muda mrefu sekta hiyo imekuwa kama imesahaulika kiasi ambacho kumekuwa na malalamiko toka kwa wananchi juu ya uwepo wa vilainishi visivyokidhi ubora

“Niseme kwakweli soko linabidhaa ambazo hazina ubora, wakati mwingine kukiri sio dhambi lakini niwahakikishie kuwa tunajipanga kuliangalia soko hili ili kuwa na bidhaa zenye viwango vinavyokubalika lakini pia kudhibiti uingizaji wa vilainishi holela hautakuwa na nafasi” Alisema

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa kiwanda hicho, Mwijage alisema kiwanda hicho kimekuja wakati muafaka na kinaenda sambambana sera ya Muheshimiwa Rais ya kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya viwanda.

“Kwa aslimia kubwa sera ya viwanda inalenga kuongeza ajira kwa wananchi wetu, Zaidi ya 75% inalenga ajira na zingine 25 ndiyo hapo mambo mengine ikiwamo kodi.
Nikiangalia hapa mnasema mtaajiri watu Zaidi ya 250, hilo ni jambo jema na kwakweli mmeunga mkono jitihada za Mh. Magufuri’ Aliongeza.

Ataka waajiri kuwaajari watumishi wao

Katika hatua nyingine, Waziri Mwijage amewataka waajiri Nchini kuacha kuwanyanyasa wafanyakazi wao badala yake wajikite kuboresha maslahi yao ili waweze kuwaombea kwa Mwenyezimungu biashara zao ziweze kunawiri.

Mwijage amesema maslahi ya mfanyakazi yakiboreshwa hata ugumu wa maisha nao utapungua na hapo ndipo mfanyakazi atatumia muda wake kujituma kwamoyo wake wote kuleta mafanikio katika viwanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Bw. Khaled Hassan Mohamedi amemshauri waziri Mwijage kuzuia uingizaji holela wa vilainishi kwani hivi sasa vilainishi vyote vinapatikana katika kiwanda hicho.


Mohamed alisema viwanda vya ndani vyakutengeneza vilainishi vya mitambo vina uwezo wa kuzalisha vilainishi hivyo kwa ubora wa hali ya juu.

Alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 45,000 za vilainishi vya aina zote na tayari wameshapata vibali kutoka kwenye taasisi mbalimbali za serikali.

“Wenye magari na mitambo wanalalamikia vilainishi visivyo na ubora sasa sisi tumekuja na bidhaa ambayo watumiaji wa vyombo vya moto wataifurahia na tutatoa waranti kama mtu chombo chake kitaharibika  kwa kutumia vilainishi vyetu tutamfidia,” alisema Mohamed.

Alisema malighafi za kutengeneza vilainishi hivyo watakuwa wanatoa nchi za Urusi, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu na kwamba Lake Lubes imewekeza Dola za Marekani milioni 4.5.

Alisema kiwanda hicho kinatarajia kuwa nafursa za ajira zipatazo 250 na mpaka sasa wameshaajiri wafanyakazi 39, kati yao 34 ni wazawa na raia wa kigeni watano na kwamba wanatarajia kuendelea kupunguza raia wa kigeni ili wabaki Watanzania pekee.

Mkuu wa wilaya akaribisha wawekezaji

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Bi Sara Msafiri amewataka wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza kigamboni wajitokeze kwani bado Kigamboni inahitaji wawekezaji vitu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment