Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na
watumishi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE (hawapo pichani)
alipofanya ziara katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam kuona namna
wanavyotekeleza majukumu yao.
.....................................
Serikali imelitaka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha
Vyuo inavyovisimamia vinahuisha mitaala yake kila baada ya miaka mitatu kwa
mujibu wa sheria ili kile kinachofundishwa kiweze kuendana na mahitaji halisi
ya soko kwa sasa ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia William Ole Nasha jijini Dar Es Salaam alipofanya ziara katika
Taasisi hiyo ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kutembelea Taasisi zilizo chini
ya Wizara na kuona namna wanavyotekeleza majukumu yao.
Ole Nasha alisema ufundi ni taaluma ambayo inabadilika kila siku hivyo ni
vyema mitaala ikapitiwa ili kozi zinazotolewa ziendana na ushindani wa soko la
ajira.
Pia Naibu Waziri Ole Nasha amelitaka Baraza hilo kuendelea kufanya
ukaguzi wa vyuo vyake na kuvifutia usajili vyuo vyote ambavyo havifuati sheria,
kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kuvichukulia hatua vinavyoendelea kufanya
makosa kwa mujibu wa sheria.
“Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) tangu mwaka 2016 imefungia
vyuo 74 ambavyo havifuati taratibu wakati mwaka huu vyuo 3 vimefungiwa huku
vingine 21 vikizuiliwa kutoa baadhi ya kozi hii ni kutokana na dhamira ya dhati
ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyo nayo ya kuhakikisha Elimu itolewayo ni bora
na sio bora Elimu” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha.
Katika hatua nyingine ameipongeza NACTE kwa kusimamia vizuri udahili wa
wanafunzi kwa mwaka huu ikiwa ni pamoja na kutengeneza mifumo 14 ya TEHAMA
ambayo imesaidia zoezi la udahili kufanyika kwa ufanisi hatua iliyopelekea
kuongeza idadi ya wanafunzi elfu kumi zaidi kutoka ile ya mwaka jana ambayo
walidahili wanafunzi 110,000.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ambayo imejipambanua katika
kufikia uchumi wa kati na wa Viwanda ambao ili uweze kufanikiwa uanahitaji
mafundi waliosoma vizuri, hivyo elimu ya ufundi ni moja ya vipaumbele vya
Serikali na kuzitaka Mamlaka hizo kusimamia elimu itolewayo ili tolewe kama
inavyostahili.
Naibu Waziri amehitimisha ziara yake ya siku moja jijini Dar es Salaam
kwa kutembelea Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi VETA ambapo
amewataka kuandaa vijana ambao ni mahiri na wabobezi katika fani mbalimbali
watakaofanya kazi katika viwanda ili kujenga uchumi wa viwanda.
Watumishi
wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) wakifuatilia hotuba ya Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha alipofanya ziara
katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es salaam.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa katika picha ya
pamoja na viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi VETA Makao makuu jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment