Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (katikati) akifunga mkutano jana wa siku
mbili wa mrejesho wa tathmini ya juu ya mambo makuu yanayowakabili Watanzania
wapya wanaoishi Ulyankulu, Mishamo na Katumba. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya
Tabora Kitwala Komanya(Kushoto) , Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama (wa
pili kutoka kushoto), Meneja wa Programu kutoka Shirika lisilo la
Kiserikali la Legal Services Facility (LSF) Ramadhan Masele(kulia) na
Mkurugenzi wa Jamii Salama Development Volunteers(JSDV) Paskali
Kilagula( wa pili kulia)
.....................................
NA TIGANYA VINCENT,RS TABORA
WALIOKUWA Wakimbizi ambao
wamepata uraia wa Tanzania wametakiwa kujifunza Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na kuzingatia sheria za Nchi ili kuepuka kujiingiza katika vitendo
vya kihalifu ambavyo vitawaondolea sifa ya kuendelea kuwa Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini
hapa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akifunga mkutano wa siku
mbili wa mrejesho wa tathmini ya juu ya mambo makuu yanayowakabili Watanzania
wapya wanaoishi Ulyankulu, Mishamo na Katumba.
Alisema Serikali haitamvumilia
raia yoyote mpya ambaye atakutwa akifanya vitendo kinyume cha matakwa ya Katiba
na Sheria za Nchi na kuongeza kuwa mtu huyo atakuwa amejitengeneza mazingira ya
kukosa sifa za kuendelea kuwa raia wa Tanzania.
“Nasema hivi ndugu zetu hao
wakitaka kuendelea kuishi hapa nchini ni lazima waishi kwa kuzingatia Katiba na
Sheria za Tanzania …kinyume cha hapa nilipata habari ya baadhi yao kuishi kwa
kuvunja Sheria zetu nitapendekeza kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
awanyang’ane uraia wale wote watakaobaika kutenda vitendo vya kihalifu”
alisema.
Mwanri aliwataka wadau mbalimbali
ikiwemo Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuendelea na utoaji wa elimu ya uraia
kwa Watanzania hao wapya ili waweze kuishi kulingana na utamaduni na desturi za
Watanzania huku waliweka mbele uzalendo na kwa kuzingatia umoja na mshikamano
ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh
Abeid Amani Karume.
Naye Meneja wa Programu kutoka
Shirika lisilo la Kiserikali la Legal Services Facility (LSF) Ramadhan Masele
alisema Watanznia hao wapya wanahitaji sana elimu ya uraia ili kuwajenga
uwezo wa kitambua sheria mbalimbali zitatumika hapa nchini kwa ajili ya
kuwafanya waishi kama walivyo raia wa asili ya Tanzania.
Alisema uelewa wa Katiba na Sheria
mbalimbali utawasaidia kuwajengea uwezo kuishi nchini bila kupotoka na
kujiiingiza katika vitendo vitakavyowatia hatiani.
Kwa upande wa Mkuu wa Makazi ya
Ulyankulu Samwel Makungu alisema utoaji wa elimu ya uraia ni muhimu sana kwa
raia hao wapya ili waweze kujua haki zao na mipaka ya haki zao kwa ajili ya
kuwafanya kuishi vizuri nchini.
Aliongeza kuwa baadhi ya raia hao
wapya wamekuwa wakikosa haki kwa sababu ya uelewa mdogo wa elimu hiyo ya uraia
na woga kwa na wengine kwa kukosa msaada wa kisheria kutoka kwa
wadau mbalimbali.
Mkutano huo wa siku mbili
uliandaliwa na Taasisi ya Jamii Salama Development Volunteers(JSDV) , Legal
Services Facility (LSF) na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi –Kitengo cha
Wakimbizi.
Baadhi
ya washiriki wa mkutano wa siku mbili wa mrejesho wa tathmini ya juu ya
mambo makuu yanayowakabili Watanzania wapya wanaoishi Ulyankulu, Mishamo
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora (hayupo katika picha ) wakati wa ufangaji
wa mkutano huo jana.
No comments:
Post a Comment