Michezo
ya Kamari imekuwa kero katika mitaa ya Bagamoyo hali inayopelekea mmomonyoko wa
maadili kwa vijana wenye umri mdogo.
BAGAMOYO KWANZA BLOG imejionea mashine hizo za
Kamari zinazojulikana kama Kamari za Mchina au DUBWI, katika mitaa mbalimbali
ya mji wa Bagamoyo.
Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG Ofisini kwake, Mwalimu
Mkuu wa shule ya Msingi Nianjema iliyopo Kata ya Nianjema Halmashauri ya
Bagamoyo, Renatus Godfrey Kisenha amekiri kuwepo kwa mchezo wa kamali jirani na
shule yake hali inayopelekea wanafunzi kushiriki mchezo huo.
Kwa kweli ndugu Mwandishi hilo swala lipo tena
hapa shuleni kwangu mashine hiyo ya Kamari ipo jirani na shule hali
inayopelekea hata watoto wa Darasa la kwanza kushiriki mchezo huo wa kamari.
Alisema kitendo cha watoto kushiriki mchezo huo kinapelekea
kuwa wezi kwa wazazi wao na walezi wao na muda mwingi akili zao zinafikiria
kucheza kamali.
Aidha ameiomba Serikali kuangalia upya leseni za
michezo hiyo ya kamali ili kulinda maadili ya vijana hasa wale ambao bado wapo shuleni
wanahitaji utulivu wa akili kujisomea.
Mzazi mmoja ambae hakutaka jina lake liandikwe
amekiri kushuhudia wanafunzi wa shule ya msingi wakicheza Kamari na kusema kuwa
wanafunzi wadogo wa Darasa la kwanza wana mudu kucheza kwasababu gharama yake
ni shilingi mia mbili tu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha
Nianjema C. Shukuru Mzuri amesema kamali imekuwa kero sio tu kwa vijana wenye
umri mdogo bali hata watu wazima ambao ni wake za watu hutumia fedha za
matumizi ya chakula kuchezea kamali na kukiri kupokea kesi kutoka kwa waume zao
juu ya tabia hiyo.
Alisema mara kadhaa amekuwa akipokea kesi za wanando kufuatia mke kushiriki kwenye kamari na kutumia fedha za matumizi ya nyumbani.
Aaidha, aliendelea kuthibitisha wizi wa fedha unaofanywa na watoto kwaajili ya kwenda kucheza kamari.
Mwenyekiti huyo alisema katika kitongoji chake
amemkabili mwenye mashine hiyo ya Kamari na imehamishwa kupelekwa mtaa
mwingine.
Kufuatia hali hiyo Kiongozi wa dini, Amiri wa
Taasisi ya Srajulmunir Islamic Center ya Mjini Bagamoyo Sheikh Abdallaah,
Kindamba, amesema kamali ni jambo lililharamishwa katika uislamu na kuiomba
serikli kupiga marufuku aina zote za kamali ili kuwalinda vijana na mmomonyoko
wa maadili na kuwajenga tabia ya kufanya kazi.
Sheikh Kindamba alisema kitendo cha kuruhusu
Kamari kila mtaa kinawafanya vijana waone kumbe unaweza kupata fedha bila ya
kufanya kazi na badala yake ukicheza Kamari unapata fedha.
BAGAMOYO KWANZA BLOG inafanya juhudi ya kuwapata
viongozi wa serikali ngazi za juu kuzungumzia hili.
No comments:
Post a Comment