Monday, October 29, 2018

KAMATI YA HUDUMA ZA JAMII YA HALMASHAURI YA CHALINZE YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO.


Kamati ya Elimu,Afya na Maji ya Halmashauri imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2018/2019.

Kamati hiyo ikiongozwa na Bi Rehema Mno ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo imeanza kwa kukagua kikundi cha Wapole Bodaboda Msata,kilichopewa milioni 4, na kununua pikipiki 2 Mwenyekiti wa kikundi Omari salum Mfikilwa ameieleza kamati kuwa kikundi kinaendelea vizuri na kitarejesha mkopo kwa wakati.

Kamati pia imetembelea Shule ya Sekondari kikaro mahali ambapo panajengwa mabweni ya wasichana kwa ufadhili wa mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Mamlaka ya Elimu Tanzania ilitoa Fedha za kitanzania Milioni 150 ambapo zitajenga mabweni mawili yenye kubeba wanafunzi 80.

Kwa mujibu wa Mwalimu wa Fedha,Naftali Sanga alieleza mbele ya kamati kuwa mpaka sasa ujenzi unaendelea na vifaa vya ujenzi vipo vyote na kuihakikishia kamati kuwa Mabweni haya yatakamilika lakini pia na nguvu za wananchi zitahitajika katika ukamilishaji wa mradi huu na hatimaye kuondoa tatizo la malazi kwa watoto wa kike katika Shule hii.

Kamati ilienda moja kwa moja katika jiko la Shule ya Sekondari kikaro la kisasa ambalo limejengwa kwa msaada wa Mapato ya ndani ya halmashauri kiasi cha shilingi Milioni 40,kutokana na Fedha hizo waliweza kujenga pia choo cha jikoni.

Mradi mwingine ulitembelewa na kukaguliwa na kamati ni mradi wa ujenzi wa madarasa mawili shule ya msingi kikaro mradi unaotekelezwa kutokana na Fedha iliyotolewa na serikali jumla ya Fedha za kitanzania Milioni 16.4,lakini kutokana na nguvu za wananchi kutumika serikali ya kijiji iliamua kuongezea chumba kimoja na kufikia vyumba vitatu.

Kamati ya huduma za Jamii imeweza kufika pia Shule tarajali ya Komkomba ambayo imejengwa na ina madarasa manne lakini haijapata usajili kutokana na kutokidhi vigezo kwa maana kwamba bado inaupungufu wa madarasa mawili,kamati imejionea ujenzi wa darasa moja lenye thamani ya Fedha za kitanzania Milioni 20.

Kwa upande wa sekta ya afya kamati ya huduma za Jamii imefika katika kijiji cha kibaoni kata ya Mandera na kuona ujenzi wa zahanati ya kijiji unaoendelea,katika ujenzi wa zahanati hii halmashauri imechangia kiasi ya Fedha za kitanzania Milioni 30,

Kamati ya huduma za Jamii ilikamilisha kazi yake kwa kutembelea na kuona ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Mwetemo,kata ya Kiwangwa, ujenzi huu unatekelezwa kutokana na Fedha zilitolewa na halmashauri kutokana na Mapato ya ndani ya halmashauri jumla ya Fedha za kitanzania Milioni 8.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa kamati ya huduma za Jamii, Mheshimiwa Rehema Mno aliwashukuru wasimamizi wa miradi katika sekta mbalimbali kwa kuonyesha moyo wa uzalendo katika utekelezaji wa miradi hiyo na kuwataka watendaji wa halmashauri kuipitia Mara kwa Mara miradi inayotekelezwa vijijini kwa ufanisi zaidi.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI, MAWASILIANO NA UHUSIANO
HALMASHAURI YA CHALINZE

No comments:

Post a Comment