Bidhaa za vyakula zenye thamani ya shilingi
milioni 93,277,368. zimeteketezwa wilayani Bagamoyo baada ya kubainika kuwa
hazina ubora kwa matumizi ya binadamu.
Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG Mkuu wa
wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa amesema bidhaa hizo zimeteketezwa kufuatia
uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kanda ya
mashariki na kubaini kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema Bidhaa hizo zimeingia
Bagamoyo kwa magendo kupitia njia ya Bahari ambapo zilikamatwa kufuatia doria
iliyowekwa na idara ya forodha wilaya kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na
Usalama wilaya.
Kufuatia hali hiyo, Mkuu huyo wa wilaya ambae pia
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, amewaonya watu wenye tabia
ya kupitisha bidhaa za magendo Bagamoyo na kusema kuwa kwa sasa wamejipanga
kudhibiti hali hiyo.
Alisema kwa sasa Kamati ya ulinzi na Usalama ya
wilaya hiyo imejiwekea mikakati mipya ya kudhibiti bidhaa zinazopitishwa kwa
njia za magendo na kusema kuwa Bagamoyo sasa sio salama kwa wapitisha magendo.
Aliongeza kwa kusema kuwa kitendo cha kuingiza
Bidhaa kwa njia za magendo ni hatari kwa maisha ya binadamu, usalama wa wilaya
yake na inaleta hasara kwa Taifa.
Akifafanua zaidi alisema Bidhaa zinazopiishwa kwa
njia za magendo zinakuwa hazikidhi vigezo vya kuingia sokoni kwaajili ya
matumizi, hivyo bila ya kudhibitiwa zinaweza kuleta madhara kwa watumiaji ambao
ni wananchi wanaotegemewa katika ujenzi wa Taifa.
Alisema licha ya kuleta madhara kwa Afya za
watumiaji lakini pia njia za magendo zinaweza kutumika hata kusafirishia
wahamiaji haramu ambao wanaweza kuleta machafuko kwa kuwa njia hizo hutumika na
watu wenye tamaa ya fedha bila ya kujali maslahi ya Taifa.
Aliendelea kusema kuwa njia za magendo hutumika
na wafanya biashara ambao wana lengo la kukwepa kulipa ushuru na kodi ya
serikali na hatimae kuzorotesha miradi ya maendeleo ambayo inategemea kodi.
Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo,
ametoa wito kwa wafanyabiashara wanaotaka kupitisha bidhaa zao Bagamoyo kutumia
Bandari iliyopo kisheria ili bidhaa hizo zilipiwe kodi na ushuru kwaajili ya
kuiingizia serikali mapato.
Alisema hatawavumilia wale wote watakaotumia njia
ambazo sio rasmi kwa lengo la kukwepa kodi na kuikosesha mapato serikali.
Alisema Bagamoyo ni mji wa kihistoria hivyo
unahitaji kuijiimarisha kiuchumi na kwamba uchumi hauwezi kuimarika bila ya
kulipa kodi zilizopo kisheria.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaagiza wakurugenzi
wa Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze kusimamia mapato ya serikali ili
kuongeza ukusanyaji wa mapato ambayo ndiyo yanayotegemewa kuleta maendeleo
katika wilaya na Taifa kwa ujumla.
Aliongeza kwa kusema kuwa, vipo vyanzo vingi
ndani ya wilaya hiyo ambavyo vikitumika vizuri Bagamoyo inaweza kujiletea
maendeleo yenyewe.
Mkaguzi wa chakula kutoka Mamlaka ya Chakula na
Dawa nchini, (TFDA) kanda ya Mashariki, Khalifa Sume amethibitisha kuwa bidhaa
hizo hazina ubora kwa matumizi ya binadamu na kusema kuwa zinapaswa kuteketezwa
ili kuepuka madhara ambayo yangeweza kujitokeza baada ya kutumia bidhaa hizo.
Khalifa alisema bidhaa hizo za vyakula
zimeteketezwa kwa mujibu wa sheria ya chakula, Dawa na Vipodozi sura Na 219 ya
Mwaka 2003 na kanuni zake za utupaji wa vyakula visivyofaa za Mwaka 2006.
Akizungumzia swala hilo Afisa Mwandamizi wa
Forodha Bagamoyo Noeli Makere alisema kukamatwa kwa Bidhaa hizo ni mpango
mkakati wa kuhakikisha mianya yote ya kukwepa kodi ya forodha ndani ya wilaya
ya Bagamoyo inadhibitiwa ili kuongeza ukusanyaji wa mapato unaotokana na Bidhaa
zinazoingia wilayani humo kwa njia ya Bahari.
Alisema Bidhaa yoyote itakayokamatwa nje ya eneo
la Bandari muhusika atapaswa kulipa kodi pamoja na faini zake zilizopo kwa
mujibu wa sheria.
Aliongeza kwa kuwataka wafanya biashara kutumia
Bandari ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza mara tu bidhaa zinapokamatwa.
Bidhaa zilizokamatwa na kuteketezwa kwa kukosa
ubore ni pamoja na Mafuta ya kupikia lita 26,840, Sukari kilo 46,300, Mchele
kilo 5,400, Maziwa lita 950 na Biskuti kilo 60 ambavyo vyote hivyo vikiwa na
thamani ya shilingi milioni 93,277,368.
Wilaya ya Bagamoyo ina jumla ya Bandari bubu
(fukwe) zaidi ya 30 ambazo hutumika kupitisha bidhaa za magendo kwa lengo la
kukwepa kulipa kodi huku baadhi yao hutumia Bandari bubu hizo (fukwe) kupitisha
wahamiaji haramu.
Mkuu wa
wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa (Mwenye miwani katikati) akiwa na watumishi kutoka Idara ya Afya, TFDA, na Idara ya forodha wakiteketeza Bidhaa za Chakula ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Afisa Mwandamizi wa Forodha Bagamoyo Noeli Makere akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG katika zoezi hilo lililofanyika hvi karibuni.
Vijana wakiendelea na zoezi la kumwaga Mafuta ya kupikia ambayo yamebainika kuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Sehemu ya Sukari na Mafuta ya kupikia vilivyoteketezwa baada ya kubainika kuwa havifai kwa matumizi ya binadamu.
No comments:
Post a Comment