Katibu,
Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutaindurwa akitoa
hotuba mbele ya Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule, Maafisa Elimu Kata na Wathibiti
Ubora (hawapo pichani) wa Manispaa ya Jiji la Dodoma katika ukumbi wa Shule ya
Sekondari Dodoma. Kulia ni Kaimu Katibu Msaidizi Wilaya ya Dodoma, Bibi Leticia
Mwakasitu na Kushoto ni Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Bw. Abdallah Membe.
....................................
Katibu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu,
Winifrida Rutaindurwa amewashauri watendaji wanaojikita katika kutoa vitisho
kwa walimu badala ya kutafuta mbinu bora za kuwasaidia kuacha kufanya hivyo ili
Walimu wasijiingize katika makosa ya kinidhamu kwa kisingizio cha kuogopa
vitisho.
Rutaindurwa ametoa kauli hiyo hivi karibuni jijini
Dodoma alipokutana na Maafisa Elimu, Wathibiti Ubora, Waratibu Elimu Kata (Maafisa
Elimu Kata), Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kutoka Halmashauri ya Jiji la
Dodoma.
Lengo la mkutano huo lilikuwa kuwaelimisha Walimu
Wakuu na Wakuu wa Shule kuzingatia maadili na nidhamu kwa mujibu wa
Sheria, Kanuni, Taratibu pamoja na Miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali.
Alisema kuwa walimu hawapaswi kuishi kwa hofu kila
wakati kutokana na vitisho wanavyopata kutoa kwa baadhi ya watendaji badala
yake wanatakiwa kutekeleza majukumu yote kwa kuzingatia misingi na taratibu za
utumishi wao.
Rutaindurwa alionesha kukerwa na baadhi ya watendaji
wanaowasimamia walimu ambao kazi yao ni kutoa vitisho vya kuwafukuza kazi au
kuwavua madakara endapo malengo flani hayatafikiwa bila kusaidia kutatua
changamoto zinazokabili Walimu kufikia malengo.
“Unakuta mtu anakuambia wanafunzi wote wasipofaulu
nakushusha cheo au nakufukuza lakini wala hamsaidii mkuu wa shule au mwalimu
mkuu kutatua baadhi ya changamoto ambazo zipo ndani ya uwezo wake” alisema.
Aliongeza kuwa vitisho hivyo vimesababisha baadhi ya
walimu kujikuta wakitenda makosa ya kinidhamu ili waonekane wamekidhi matakwa
ya wanaowasimamia na matokeo yake wanachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo
kufukuzwa kazi.
“Sasa walimu lazima mtumie akili na sio kufanya vitu
ili umridhishe mtu wakati unajiingiza katika hatari. Ukienda kuiba mtihani na
kuwapa majibu wanafunzi ili ionekane shule yako imefanya vizuri hautabaki
salama” alisema.
Aliongeza kuwa, “napenda muelewe kuwa ukitenda kosa
usifikirie utakuja kujitetea kwa kusema nilifanya kwa vile niliambiwa nikaogopa,
sisi tunakushughulikia wewe uliyekiuka maadili na taratibu za ualimu,
unawajibika mwenyewe.”
Amesisitiza kuwa ni lazima mwalimu atekeleze wajibu
wake kikamifu katika kufundisha ili wanafunzi wafaulu lakini baadhi ya
watendaji nao hawapaswi kutoa vitisho vinavyomfanya mwalimu ashawishike kutenda
makosa ili tu afikie malengo.
“Nimefurahi kwa kuwa Maafisa Elimu na Wathibiti
Ubora mpo hapa. Nipende kuwasihi msiwatishe walimu kupita kiasi, wengine
wanawatishia kuwafukuza kazi wakati mamlaka hayo hawana. Tuwahimize
walimu kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia taratibu zinazotakiwa lakini
tusipende kuwatwisha mizigo isiyoendana na uhalisia.
Aliongeza kuwa suala la kukuza elimu sio jukumu la
mwalimu peke yake bali jamii wakiwemo viongozi, wazazi na walezi katika maeneo
yao wana sehemu kubwa kusaidia kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha
wanafunzi kufaulu.
“Wapo baadhi ya wazazi ambao hawafuatilii maendeleo
ya watoto wao kabisa, wapo wengine ambao bado wanawafundisha watoto kuandika
majibu ya uongo ili wasifaulu. Sasa hapa ni lazima viongozi kama madiwani na
wengine wajitahidi kuwaelimisha wazazi ili waunge mkono juhudi za kuinua
kiwango cha elimu”, alisema.
Alihitimisha kuwa Tume ya Utumishi wa Walimu ina
wajibu wa kuwaelimisha walimu ili wasijihusishe na makosa ya kinidhamu katika
utumishi wao na sio kwamba kazi kubwa ya Taasisi hiyo ni kusubiri walimu
watende makosa ili iwafukuze kazi.
Walimu
wakiwa katika hali ya utulivu wakimsikiliza Katibu, Ofisi ya Rais, Tume ya
Utumishi wa Walimu, Winifrida Rutaindurwa (hayupo pichani) akiwaelimisha juu ya
Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu.
Walimu
Wakuu na Wakuu wa Shule wa Halmasahauri ya Jiji la Dodoma wakiwa katika hali ya
furaha wakati wa Mkutano wao na Katibu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa
Walimu, Winifrida Rutaindurwa ( hayupo pichani) uliofanyika jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment