Tuesday, October 23, 2018

SHULE YA SIRAJULMUNIR BAGAMOYO YASHIKA NAFASI YA KWANZA MKOA WA PWANI.

Wanafunzi waliohitimu elimu ya Msingi shule ya Msingi Sirajulmunir Bagamoyo wakiwa na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Sirajulmuni ambayo ndiyo inayomiliki shule hiyo Baraka Kalangahe (kulia) na Meneja wa shule hiyo Mwarabu Pyalla (kushoto)
 
Wanafunzi waliohitimu elimu ya Msingi shule ya Msingi Sirajulmunir Kiwangwa siku ya Mahafali yao.
.................................


Shule ya msingi Sirajulmunir Bagamoyo yashika nafasi ya kwanza Mkoa wa Pwani matokeo ya Darasa la saba 2018.

Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG kwa njia ya simu, Meneja wa shule za Sirajulmunir Mwarabu Piyalla  amesema amefarijika na matokeo hayo ambayo kiukweli ni ya kujivunia.

Alisema shule ya Msingi Sirajulmunir Bagamoyo imekumbwa na changamoto kadhaa hasa wakati wa kipindi cha mvua ambapo shule hiyo ilijaa maji na kulazimika kuhama kwa muda jambo ambalo liliwathiri watoto kitaaluma kutokana na mazingira ya kusomea.

Aliongeza kwa kusema kuwa licha ya changamoto hizo walimu waliweza kushirikiana vyema na wazazi katika kuhakikisha kiwango cha taaluma kinapanda na sio kushuka.

Mwarabu Pyalla ambae kitaaluma ni mwalimu alisema miongoni mwa changamoto za uendeshaji wa shule ni pamoja na ulipaji wa ada ambapo wazazi na walezi wanashindwa kulipa ada kwa wakati hivyo kitendo cha kumpa barua mtoto kwamba anadaiwa ada ni miongoni mwa mambo yanayomuathiri kisaikolojia na kitaaluma.

Akielezea matokeo ya Darasa la saba kwa shule za Sirajulmunir alisema Shule ya Sirajulmunir Bagamoyo iliyopo Kata ya Nianjema Halmashauri ya Bagamoyo, ilkuwa na wanafunzi 30 waliofanya mtihani na kushika nafasi ya kwanza kati ya shule 16, zilizopo Halmashauri ya Bagamoyo katika kundi la shule zenye wanafunzi chini ya 40, huku ikishika nafasi ya kwanza pia Mkoa wa Pwani kati ya shule 323 zilizopo Mkoa wa Pwani zilizo kundi la wanafunzi chini ya 40. na kushika nafasi ya 33 kitaifa kati ya shule 6726.

Aliendelea kusema kuwa shule ya Sirajulmunir Kiwangwa iliyopo kata ya Kiwangwa Halmashauri ya Chalinze, ilikuwa na wanafunzi 8 imeshika nafasi ya 1 kati ya shule 57 zilizopo Halmashauri ya Chalinze kwenye kundi lenye wanafunzi chini ya 40 huku ikishika nafasi ya 7 Mkoa wa Pwani kati ya shule 323 na nafasi ya 137 kitaifa kati ya shule 6726.

Mwarabu Piyalla alisema shule ya Sirajulmunir imepata wastani wa 221.8333 huku Sirajulmunir Kiwangwa ikiwa na wastani wa 210.7500.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mwenyezimungu kwa hatua hiyo huku akiwapongeza walimu kwa kazi nzuri wazazi na walezi kwa ushirikiano wao na viongozi wa Taasisi inayomiliki shule hizo kwa juhudi zao za kuhakikisha shule hizo zinaendelea kutoa elimu kwa vijana.

Shule za Sirajulmunir zinamilikiwa na Taasisi ya Sirajulmunir Islamic Center yenye makao yake Makuu Majani mapana mjini Bagamoyo.

Shule ya Sirajulmunir Bagamoyo ina jumla ya wanafunzi 265 na Sirajulmunir Kiwangwa ina jumla ya wanafunzi 132 ambapo Meneja Mwarabu Pyalla alitoa kwa wazazi na walezi kuwahi mapema kuchukua fomu za kujiunga na shule hizo ambazo zina walea watoto kiroho na kimwili na kuwajenga katika misngi ya maadili mema itakayosaidia katika ngazi ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa mawasiliano na shule za Sirajulmunir unaweza kuwasiliana kwa namba za simu +255(0)712436036 au +255(0)719569037.



Matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi (darasa la saba) kwa mwaka 2018 yametangazwa leo Oktoba 23 2018, ambapo matokeo yanaonyesha ongezeko la ufaulu kwa asilimia 4.76% tofauti na ufaulu wa 2017 ambao ulikuwa asilimia 72.76%.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Dkt. Charles Msonde, amesema katika tathmini ya awali kiwango cha ufaulu kimepanda kwa asilimia 4.9% ikilinganishwa na 2017, amesema pia kiwango cha ufaulu wa somo la Kiingereza uko chini sana tofauti na masomo mengine (50%).

NECTA pia limewafutia matokeo watahiniwa 357 waliobainika kufanya udanganyifu kwenye mitihani iliyofanyika mwaka huu 2018.
“Baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa zaidi 100 kutokana na kuugua kipindi cha mtihani na kuwapa fursa ya kufanya mtihani huo mwaka 2019,” amesema Msonde.

 

Picha inayo onesha matokeo ufaulu kwa kila mwanafunzi kwa shule ya Sirajulmunir Bagamoyo. 
  
Picha inayo onesha matokeo ufaulu kwa kila mwanafunzi kwa shule ya Sirajulmunir Kiwangwa.

Kuangalia matokeo ya jumla kwa shule zote nchi nzima bonyeza hiyo link chini.

NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA

PSLE-2018 EXAMINATION RESULTS





 

No comments:

Post a Comment