Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wanafunzi
kuwa na maadili mema, kufuata sheria na taratibu za nchi na kuachana na
matendo yote yanayokiuka maadili ikiwemo wizi wa mitihani.
Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyampulukano iliyopo
wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Jaji Mkuu aliwaambia wanafunzi hao kuwa wizi
wa mitihani ni tatizo la kwanza la ukosefu wa maadili katika jamii.
Aliwataka wanafunzi hao kujenge tabia ya kujisomea mambo mbalimbali kwa kuwa
karne hii ya ishirini na moja ni karne ya sayansi na teknolojia yenye taarifa
nyingi zitakazowasaidia kwa maendeleo yao.
“Karne hii ya ishirini na moja ni tofauti na karne ya ishirini, someni
mambo mbalimbali ili mfahamu nchi yenu inakwendaje”, alisema Jaji Mkuu huku
akiwasisitiza waisome Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili wafahamu
Tanzania itakuwa ni nchi ya namna gani.
Aidha, Jaji Mkuu pia aliwashauri wanafunzi watakaopenda kuwa wanasheria
hapo baadaye kuhakikisha wanakuwa waadilifu katika jamii kwa kuwa fani ya
sheria inahitaji mtu aliye na maadili mema hasa na yule anayechukia na
kuvipinga kwa nguvu zote vitendo vya rushwa.
Hata hivyo alisema kutokusoma sheria hakutawazuia kufahamu sheria
mbalimbali za nchi na kuwa karne hii ya ishirini na moja inahitaji fani zote
kushirikiana ili kuwa na maendeleo.
Akizungumzia rushwa na uchumi wa nchi, Jaji Mkuu alisema ziko nchi
duniani zenye rasilimali nyingi na zimeweza kubadili maisha ya raia wake na
wakati huo huo zipo nchi zenye rasilimali nyingi lakini hazijaweza kubadili
maisha ya watu wake kutokana na rushwa hivyo aliwataka wanafunzi hao kukataa
rushwa kwa kuwa ni adui wa maendeleo yao.
Mahakama ya Tanzania imeanzisha mpango wa kuzitembelea shule mbalimbali
nchini kwa lengo la kuwaandaa vijana kuwa na maadili mema katika jamii wakiwamo
wanasheria wa baadaye.
Jaji Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Mwanza ambapo
anakagua shughuli za mahakama kwenye Mahakama zilizopo mkoani humo.
No comments:
Post a Comment