Thursday, October 25, 2018

WANANCHI WA CHALINZE WAHAKIKISHIWA KUPATA MAJI APRIL 2019-SAMIA.


NA MWAMVUA MWINYI, CHALINZE 

SERIKALI imewahakikishia wananchi wa jimbo la Chalinze ,mkoani Pwani kuwa wataondokana na tatizo la maji na kubaki historia ifikapo mwezi april mwakani. 

Tatizo la maji limekuwa likiwapa shida wananchi hao kwa miaka mingi hali iliyokuwa ikiondoa imani na serikali yao. 

Akizungumza na wakazi wa Chalinze, makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu alisema ,shida ya maji Chalinze imekuwa kubwa ambapo wamekuwa wakikosa huduma hiyo ya maji safi na salama ya uhakika. 

“Tukiahidi tunatekeleza, na serikali mkiiona haitekelezi baadhi ya mambo kwa haraka lazima inasababu na inatolea ufafanuzi wa kusuasua kwa jambo husika “
“Faraja inakuja, naimani ifikapo 2019 kero hii itakuwa historia, “alisisitiza. 
Pamoja na hayo, Samia amewataka akinamama wajawazito wakiwa tayari kujifungua wakimbilie hospital ama vituo vya afya badala ya kuendekeza masuala ya kishirikina suala linalosababisha vifo kwa mama na mtoto. 

Aliwaomba ,watumie vituo vya afya kunusuru vifo vya akinamama na watoto. 

Akizungumzia tatizo la mgogoro wa wakulima na wafugaji aliwaasa waheshimiane. 

Akitolea ufafanuzi juu ya kudhibiti tatizo hilo, naibu waziri wa mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega alisema, NARCO inaanzisha maeneo ya wafugaji na imetenga heka 100,010 ambapo ng’ombe watahamishia malisho ndani ya Narco.

“Miezi mitatu ng’ombe mmoja atalipiwa sh. 10,000 na ukiisha muda huo unaanza mkataba upya”alielezea.

Ulega alifafanua, njia hiyo itapunguza ongezeko la mifugo hiyo.
Alieleza itakuwa ni ofa kwa wafugaji kunenepesha ng’ombe wao kwenye shamba hilo la serikali. 

Awali mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete alieleza changamoto ya kero ya maji ni kubwa kwa kipindi kirefu. 

Anasema ,uchelewaji wa hatua za kupata huduma ya maji inaleta sura ya kufanya siasa kwa wananchi ambao bado wanaiamini serikali yao. 

Ridhiwani aliiomba, serikali kuendelea kusukuma na kuusimamia mradi wa CHALIWASA ili uanze kazi haraka na kuondoa kero hiyo.

No comments:

Post a Comment