Picha
mbalimbali za ziara ya Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi na
Ujumbe wake Beijing, China inaendelea ambapo ametembelea Vyombo vya Habari vya
People’s Daily na China Daily.
.................................
Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, CHINA
Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Hassan Abbasi Jumatano Oktoba 24, 2018 ametembelea magazeti ya People’s
Daily Online na China Daily nchini China kwa lengo la kujifunza na
kujadiliana namna bora zaidi ya kushirikiana katika sekta ya habari.
Akiwa katika vyombo hivyo, Dkt. Abbasi amesema kuwa China na
Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu kwenye masuala mbalimbali hivyo
ni muda sasa wa kufanyia kazi mkataba wa ushirikiano wa Tanzania na China
kwenye masuala ya utamaduni na habari uliosainiwa mwaka 2016
“Lengo la ziara yetu ni kujifunza wenzetu mnavyofanya kazi na pia
kutafuta namna ya kuweza kufanya kazi kwa pamoja katika sekta ya habari,”
ameongeza Dkt. Abbasi akiwa People’s Daily.
Amelitaka gazeti hilo linalomilikiwa na Chama cha Kikomunisti cha China
(CPC) na linalofikisha habari zake kwa wasomaji milioni 700 duniani
kupitia mitandao mbalimbali kuenzi ushirikiano huo wa muda mrefu kwa kuzipa
nafasi pia habari za maendeleo za Afrika na Tanzania.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), Bw.
Pascal Shelutete amewakumbusha viongozi wa chombo hicho kuzipa fursa habari za
utalii hasa vivutio vingi vilivyoko Tanzania.
Akiwa katika gazeti la China Daily lililoanzishwa na Serikali ya China
zaidi ya miongo mitatu iliyopita, Dkt. Abbasi aliwaeleza wahariri wanaohusika
na toleo maalum la Afrika kuzingatia kuwa nchi nyingi za Afrika hasa Tanzania
zina maendeleo na vivutio vya uwekezaji vinavyopaswa kujulikana kwa
wekezaji wengi wa China maombi ambayo wahariri wa gazeti hilo waliyakubali.
Dkt. Abbasi anaendelea na ziara yake ambapo atatembelea television za
China za CCTV na CGTN na baadaye kufanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya
Redio China.
No comments:
Post a Comment