Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa kijiji cha Lukozi wilayani
Lushoto wakati alipowasili kijijini hapo akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga,
Oktoba 31, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
......................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria
kuboresha huduma za afya kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya
halmashauri ya wilaya ya Lushoto.
Amesema lengo ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye
uwezo wa kutoa huduma mbalimbali muhimu zikiwemo za maabara, upasuaji na mama
na mtoto.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Oktoba 31, 2018) wakati akizungumza na
wakananchi katika kata ya Malindi, baada ya kutembelea jengo la soko mbogamboga
la Malindi.
Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga vizuri katika sekta ya afya baada
ya bajeti ya kununulia dawa kuongezeka kutoka sh. bilioni 31 kwa mwaka na
kufikia bilioni 269.
“Hatutaki tena kusikia mgonjwa anaenda hospitali na kukosa dawa biashara
hiyo tumeimaliza, Rais Dkt. John Magufuli ametoa fedha nyingi kwa ajili ya
ununuzi wa dawa.”
Amesema katika wilaya ya Lushoto Serikali imetenga sh. bilioni 1.4 kwa
ajili ujenzi na ukarabati wa majengo ya vituo vya afya vya kata za Kangagai.
Mnazi na Mlola.
“Halmashauri wekeni mpango thabiti wa kujenga wodi mbili kati yake moja
ya wanaume na nyingine ya wanawake, lengo la Serikali ni kuboresha huduma za
afya kwa wananchi.”
Aizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa soko, Waziri Mkuu amesema mradi huo
ni sehemu ya huduma zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za
jamii nchini.
Waziri Mkuu ametaja huduma nyingine zinazotolewa na Serikali kwa wananchi
ni za afya, elimu, maji, uchumi na ujenzi na uboreshwaji miundombinu mbalimbali
ikiwemo ya barabara.
Hivyo, amewataka wananchi watumie vizuri soko hilo ambalo
linatoa fursa kwao kufanya biashara katika eneo zuri na kuwawezesha kuuza
bidhaa zao zikiwa katika ubora.
Pia amewashauri wakulima hao wajiunge katika vikundi na kuanzisha
ushirika wao ili waweze kusaidiwa na Serikali katika kupata mikopo kwa ajili ya
kuzalisha kwa ubora zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Bibi
Ikupa Mwasyoge amesema kukamilika kwa soko hilo kutainufaisha halmashauri na
wananchi.
Bibi. Ikupa amesema ujenzi wa jengo hilo la soko la ghorofa mbili
lililojengwa kwa awamu mbili ulianza mwaka 2011 na umekamilika Septemba 2018,
umegharimu sh. bilioni 1.1.
Amesema halmashauri itanufaika kwa kupata ushuru na wananchi ambao wengi
wao ni wakulima wa mboga na matunda watakuwa na sehemu ya uhakika wa kufanyia
biashara.
“Wakulima 35,000 wa kata ya Malindi na kata jirani za Lukozi, Manolo na
Shume wanaozalisha wastani wa tani 5,900 za mboga na matunda kwa mwaka
watanufaika.”
Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za afya
nchini.
Amesema bajeti ya dawa katika halmashauri hiyo imeongezeka kutoka sh
milioni 183 za dawa zilizokuwa zinatolewa awani na sasa imefikia sh milioni
565.
Mbunge wa jimbo la Mlalo, Bw. Rashid Shangazi ametumia fursa hiyo
kuishukuru Serikali kwa kuwasaidia wananchi wa halmashauri kuongeza thamani ya
mazao yao kabla ya kuuza.
Awali,Waziri Mkuu alizindua jengo la utawala la Halmashauri ya wilaya ya
Lushoto lililogharimu sh. bilioni 4.3. Kukamilika kwa jengo hilo kutaboresha
huduma kwa wananchi.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua Jengo la Halmashauri ya
Wilaya ya Lushoto akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga Oktoba 31, 2018.
Kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu na wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano
na Mazingira, January Makamba. Wapili kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa
Tanga, Henry Shekifu, watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.
na kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Ikupa Harrison
Mwasyoge. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Soko la Kisasa la mbogamboga na
matunda linalojengwa na Serikali katika kijiji cha Malindi wilayani Lushoto,
Oktoba 31, 2018. Alikuwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga. Wapili kulia ni
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment