Thursday, October 18, 2018

NAIBU WAZIRI KAKUNDA AIPONGEZA DYCCC.

Naibu Waziri Pfisi Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Joseph Kakunda akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa Darasa la saba na kidato cha sita wa shule za Yemen DYCCC. Chang'ombe Jijini Dar es Salaam.
..................................................

Shirikia la DYCCC linalomiliki shule za Yemen zilizopo Chang'ombe Jijini Dar es Salaam limepongezwa kwa kuwa na majengo mazuri ya kimataifa ambayo yanaakisi elimu inayotolewa hapo.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri Pfisi Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Joseph Kakunda alipokuwa akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa Darasa la saba na kidato cha sita wa shule za Yemen DYCCC. Chang'ombe Jijini Dar es Salaam.

Alisema kutokana na mazingira mazuri ya shule hiyo ni wazi kuwa mtoto atashawishika na kupenda kusoma hali inayosaidia katika usimamizi wa wanafunzi wasiopenda kusoma.

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa anaamini elimu inayotolewa shuleni hapo ni bora inayokidhi viwango vya elimu vya kimataifa kama yalivyo majengo hasa pale aliposhuhudia maonesho ya watoto hao walipokuwa wakionesha kile walichojifunza.

Shule hizo za Yemen DYCCC ambazo zinafundisha na maarifa ya uislamu wanafunzi waliweza kumuonesha mgeni rasmi mambo mbali waliyojifunza shuleni hapo ikiwa ni pamoja ufahamu wa mambo ya kiislamu, masomo ya Sayansi, na Hesabu huku wakionesha namna walivyofundishwa kuwa na maadili mema katika jamii.

Kufuatia hali aliyojionea Naibu waziri huyo wa TAMISEMI alisema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Taasisi za dini na mashirika binafsi, na mtu mmoja mmoja  katika uwekezaji unaofanywa kwenye sekta ya elimu hapa nchini.

Naibu Waziri Kakunda alisema katika kuboresha elimu hapa nchini serikali imetoa fursa kubwa kwa watu binafsi, mashirika ya dini na yale ya binafsi kuwekeza katika elimu  na hatimae Taifa lipate wataalamu watakaoendesha kampuni za ndani ya nchi ili kwenda sambamba na utekelezaji wa sera ya viwanda.

Alisema hivi sasa Tanzania inatekeleza sera ya Viwanda hapa nchini lakini katika ujenzi wa Viwanda na miundombinu mbalimbali inayojengwa na Serikali Baadhi ya Kampuni ni za kigeni ambazo zimekuja na wataalamu wake.

Aliongeza kuwa ifike wakati watanzania wawe na elimu ya kuendesha mambo mbalimbali ikiwemo uhandisi wa majengo ili kusimamia na kujenga miundombinu yetu kwa viwango vinavyokubalika kitaalamu.

Aliendelea kusema kuwa, anaamini mashirika kama ya DYCCC yanawajenga vizuri vijana kitaaluma na maadili mema na kuahidi kushirikiana nao ili kuboresha kiwango cha taaluma hapa nchini.

Aidha, amelishauri shirika la DYCCC kuanzisha elimu ya ufundi na chuo kikuu ili vijana waweze kujiendeleza katika fani mbalimbali chini ya usimamizi wao.
Naibu Waziri Kakunda alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wanafunzi wote hapa nchini kutilia mkazo kwenye masomo ya Sayansi na Hesabu ili kukidhi mahitaji ya wafanyakazi katika sekta ya viwanda.

Katika hutuba yake aliwataka vijana wahitimu wa elimu ya msingi na kidato cha sita kujiwekea malengo ya kuendelea na elimu kwani elimu ya msingi ni mwanzo tu wakutafuta elimu na kuwaonya waepuke vishawishi vya mitaani ili wasivuruge malengo yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya elimu ya shule za DYCCC Hassan Akrabi aliwataka wazazi kutoa ushirikiano kwa walimu ili kufikia malengo ya kuwa vijana elimu iliyo bora.

Akrabi alisema shule za DYCCC zina wale vijana katika maadili mema hivyo ni vyema wazazi nao wakaendeleza kile watoto wao walichokipata wakiwa katika shule hiyo.

Aliongeza kwa kusema kuwa shule za DYCCC ambazo ni Shule ya awali, Msingi na Sekondari zimejipanga katika kuinua kiwango cha ufaulu na ili vijana wanaotoka katika shule hizo wawe na uwezo wa kuendelea sehemu yoyote.

Awali akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi, Meneja wa shule za DYCCC Jamila Awadhi, alisema shule za DYCCC zinaendela kutoa elimu inayokidhi viwango ambapo wahitimu wake  wamekuwa na uwezo wa kujiunga na elimu za juu ndani na nje ya nchi.

Alisema lengo la shule ni kuwaelimisha na kuwalea vijana kiroho, kimwili na kiakili kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita katika maadili bora ya uislamu yanayozingatia haki na uadilifu ili waweze kuwa raia wema watakaoleta maendeleo ya familia zao na Taifa kwa ujumla.

Aidha, alitaja changamoto mbalimbali zinazokabili shule hizo ikiwa ni pamoja na kutofautiana kimtazamo na baadhi ya wazazi, kupanda kwa gharama za uendeshaji wa shule hali inayopelekea kutumia nguvu ya ziada kuweza kufanikisha hayo.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi Mwenyekiti wa kamati ya wazazi wa shule hiyo, Dr. Abdallaah Tego aliwataka wazazi kubadilika na kuifunza mbinu za malezi ili kwenda sambamba na Teknolojia ambayo imeweteka watoto wengi.

Alisema ni vyema wazazi na walezi wakajifunza mbinu za malezi kitaalamu ambapo itawasadia kwenda na hali halisi ya ulimwengu katika kulea watoto.
Shule za Yemen zinazomilikiwa na DYCCC zina jumla ya wanafunzi 1,353 ambao ni pamoja wanafunzi wa shule ya awali, Msingi, kidato cha nne na sita.
  
Mwenyekiti wa Bodi ya elimu ya shule za DYCCC Hassan Akrabi akizungumza katika mahafali hayo yaliyofanyika hivi karibuni.
 
Meneja wa shule za Yemen DYCCC Jamila Awadhi, akizungumza katika mahafali hayo. 
 
Mwenyekiti wa Bodi ya elimu ya shule za DYCCC Hassan Akrabi akimuonesha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Joseph Kakunda majengo yaliyopo shuleni hapo yalikuwa upande wa kushoto wa meza kuu.
 Majengo ya Shule za Yemen DYCCC zilizopo Chang'ombe Jijini Dar es Salaam.

 
Wanafunzi wa shule za Yemen DYCCC wakionesha mambo mbalimbali waliyofundishwa shuleni hapo.
 
Mwalimu Rahimu ni Mkuu wa Shule ya Msingi Yemen DYCCC.

No comments:

Post a Comment