Mkuu
wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo (wa katikati) akizungumza kuhusu ujio
wa makamu wa Rais mkoani humo, (wa kwanza kushoto) katibu tawala mkoa Theresia
Mbando na wa kwanza kulia kaimu mkuu wa wilaya ya Kibaha Jokate Mwegelo.
.........................
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu
anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi Mkoani Pwani octoba 24 ambapo
atatembelea miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa Bandari mpya ya
Bagamoyo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Mhandisi Evarist Ndikilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari .
Ndikilo alisema ,makamu wa Rais akiwa mkoani humo atakagua
miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya nne za
mkoa huo na ataanzia ziara kwa kukagua miradi ya maendeleo ya Wilayani
Bagamoyo.
“Miradi hiyo ni pamoja na kutembelea mradi mkubwa wa
Bandari mpya ya Mbegani wilayani Bagamoyo yenye ubia na nchi tatu
za Tanzania,Oman na China,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa baada ya kukagua miradi wilayani Bagamoyo
atakwenda Halmashauri ya wilaya ya Chalinze ambako atakagua miradi
ya maendeleo.
“Baada ya hapo atakwenda , Wilaya ya Kisarawe, Mkuranga na
atahitimisha ziara hiyo wilaya ya Kibaha”
Aidha mradi mwingine wa kitaifa ni atakaotembelea ni ujenzi wa reli ya
kisasa ya Standard Gauge (SGR) kwenye karakana kubwa iliyoko Soga wilayani
Kibaha.
“Mbali ya kutembelea miradi hiyo mikubwa pia atatembelea miradi mingine
ikiwemo ya miradi ya afya, maji na elimu,”alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa akiwa wilayani Kibaha Makamu wa Rais anatarajiwa
kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonyesho ya wiki ya viwanda
itakayozinduliwa Oktoba 29 katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika
eneo la Picha ya Ndege.
Makamu wa Rais atakapoanza ziara hiyo atapokea taarifa kutoka
Halmashauri zote za mkoa huo pia atapata nafasi ya kuzungumza na
Wakurugenzi wa Halmashauri hizo.
No comments:
Post a Comment