Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine
Ndugulile akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa Diwani wa Kinyambuli Rubeni
Charles wakati alipofanya ziara katika kijiji hicho ili kujionea hali ya ujenzi
wa kituo pamoja na utoaji huduma za afya kijijini hapo.
..........................................
Na WAMJW-MKALAMA,SINGIDA
Watanzania kote nchini wametakiwa kufuata kanuni na taratibu bora za
maisha ikiwemo kubadili mfumo wa maisha ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya
kuambukiza pamoja na udumavu kwa watoto wachanga.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika Wilaya ya Mkalama Mkoa wa Singida
wakati alipotembelea kituo cha afya na kuongea na wananchi.
“Serikali chini ya uongozi wa Rais Magufuli inataka kila mtanzania awe na
afya bora, ndo maana tunajitahidi kutoa elimu kwa umma kuhusiana na kutunza
afya zenu ikiwemo kufanya mazoezi na kuepuka vyakula ambavyo si salama kwa afya
zetu pamoja na kubadili mfumo mzima wa maisha”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha,Naibu waziri huyo ameendelea kusisitiza kwa upande wa akina
mama walio na watoto wadogo chini ya miaka miwili kuendelea kuwanyonyesha na
kuwapa vyakula vyenye lishe bora watoto wao ikiwa ni sehemu ya kumsaidia mtoto
kukua kiakili na kuwa na afya bora huku akisisitiza siku 1000 za mwanzo
kwa mtoto ndizo siku muhimu katika kumuwezesha kuwa na afya bora na kukua
vizuri.
“Siku 1000 za mwanzo tunaanza kuzihesabu toka mimba inapotungwa,
anapozaliwa na kufikisha miaka miwili, hiki ni kipindi muhimu sana cha mama
kumnyonyesha mtoto ikiwa ni pamoja na kumpa vyakula vyenye lishe ili mtoto aweze
kuwa na afya bora na ubongo unaofanya kazi sawa sawa”. Alisisitiza Dkt.
Ndugulile.
Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile amekipongeza kituo cha afya cha Kinyambuli
kwa kuzitendea haki fedha zilizotolewa na Serikali Shilingi milioni 400 ili
kusaidia kupanua kituo hicho kwa kujenga majengo mapya ya kuhudumia wagonjwa
pamoja na nyumba za watumishi.
“Nawapongeza sana wananchi wa Kinyambuli kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa
kituo hiki, ninachokiona hapa kipo mara 300 nchi nzima, kwa kweli mnastahili
pongezi na fedha za serikali tulizoleta milioni 400 mmezitendea haki”. Alisema
Dkt. Ndugulile.
Hata hivyo Dkt.Ndugulile amesema serikali bado ina nia kubwa ya
kuboresha hali ya utoaji huduma za afya nchini, huku ujenzi wa Hospitali kubwa
ya wilaya ya Mkalama ukitarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Dkt. Ndugulile amesema mkoa wa Singida umetengewa bajeti ya Bilioni 1.5
kwa ajili ya kujenga Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama pamoja na Singida DC.
Kwa upande wake diwani wa Kinyambuli, Rubeni Charles ameishukuru serikali
ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa kuwakumbuka
wananchi wa kijiji hicho kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo kikubwa cha afya.
“Kwakweli naishukuru sana serikali kwa kutukumbuka, wananchi wa kijiji
hiki walikua wanapata shida sana kupata huduma za afya hasa wakinamama
wajawazito ambao tulipoteza wengi kutokana na kukosa huduma hii muhimu”.
Alisema Rubeni.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine
Ndugulile akinawa mikono baada ya Uzinduzi wa Mradi Mkubwa wa Maji wenye
uwezo wa kuzalisha lita za ujazo Elfu 30 kutoka kijiji cha
Rurumakilichopo kata ya Kiomboi wilaya ya Ilamba, ikiwa ni muendelezo wa zaiara
yake Mkoani Singida.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine
Ndugulile akiangalia chanjo zilizohifadhiwa katika boksi maalum wakati alipotembelea
Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi iliyopo wilayani Iramba katika Mkoa wa Singida.
Kushoto ni muhudumu wa chanjo Christowelo Palangyo na Dkt. Abbas Sepoko
(kulia).
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine
Ndugulile akiionesha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Iramba (hawapo
pichani) dawa za serikali zilizo na alama maalumu ili zisiuzwe katika maduka
binafsi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Gwaula.
No comments:
Post a Comment