NA MWAMVUA MWINYI,CHALINZE
KAMATI ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo, haijaridhishwa
na kushuka kwa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ya Chalinze, kipindi cha
mwaka 2017/2018 ,na kuiasa iongeze jitihada ili kuinua ukusanyaji huo.
Kwa miaka miwili mfululizo Halmashauri hiyo imesifika kwa ukusanyaji
mzuri unaovuka malengo lakini kwa taarifa kutoka wizara ya TAMISEMI inaonyesha
haimo kwenye Halmashauri bora kwa ukusanyaji wa mapato .
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Abduli Zahoro Sharif alisema
,wamelazimika ,kukutana na wakuu wa idara, wataalamu na madiwani wa
Halmashauri hiyo, kuangalia endapo kuna mapungufu ama mianya
yaliyosababisha kushuka kwa makusanyo hayo ili yadhibitiwe .
“Usimamizi sio mzuri katika makusanyo hali inayosababisha kushuka kwa
makusanyo Halmashauri ya Chalinze na kushuka kuwa nafasi ya tatu kimkoa kutoka
nafasi ya kwanza “
“Achani kufanya kazi kimazoea na bado sijaridhishwa na hali ya makusanyo
na mtasababisha ilani kushindwa kutekelezeka kwa wakati ,alisema Alhaj Sharif.
Aliwataka washirikiane baina ya wataalamu, watendaji na madiwani kwa
pamoja kubuni vyanzo vipya vya mapato.
“Tuna taarifa zipo, posi (EFD) 80 lakini wanatumia posi 30 ,na eneo
ambalo ndio chanzo kikuu cha makusanyo ni ushuru wa kokoto ambapo hawatumii
posi wanatumia karatasi wanazoziita vocha.” alifafanua Alhaj Sharif.
Kwa upande wake ,Mweka hazina wa Halmashauri ya Chalinze (DT) David
Rubibira alisema kwa siku moja wanakusanya makusanyo katika malori ya kokoto
197-200 ambapo kwa siku wanakusanya sh.mil.8.9 .
Ofisa mipango wa Halmashauri ya Chalinze ,Shabani Millao alisema ,kuhusu
suala la kushuka kwenye makusanyo ya mapato ya Halmashauri hiyo linatafsirika
sivyo kwani wapo vizuri katika makusanyo .
Millao alitaja sababu za kutofikia kwenye makusanyo kwa kipindi hiki kuwa
ni pamoja na kushushwa kwa makusanyo ya mazao ya chakula yasiyozidi tani moja
,na kuzuiwa kwa ushuru wa mabango .
Alisema ,wamejipanga kurekebisha makadirio kutegemeana na hali halisi ya makusanyo
kulingana na chanzo husika.
Kwa upande wake ,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Saidi Zikatimu
alifafanua ,ukusanyaji 2016/2017 walikusanya kiasi cha shilingi Bilioni 3.800 wastani wa asilimia 118.
“Tukaona kama tumevuka lengo tukaona tujiwekee malengo ya juu na tuongeza
ongezeko la asilimia 26 ambalo tumekusanya sh.Bilioni 4 badala ya kukusanya Bilioni
4.3″alisema Zikatimu.
Alisema, katika malengo ya mwaka huo walivuka lengo kwa kukusanya kwa
asilimia 17 badala ya asilimia 26 .
Zikatimu alielezea ,wameanza kujipanga kusaidia na idara ya fedha ili
kufikia malengo wanayojiwekea ,ambapo kwa mwaka huu wameshajiwekea Bilioni tano
ambalo ni ongezeko la asilimia 30.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ,Amina Kiwanuka alisema wamepokea maagizo
yaliyotolewa na kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha makusanyo.
No comments:
Post a Comment