Waziri
wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akipanda mti kwenye chanzo cha Mtawanya, Mtwara
Mjini.
.........................
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa leo amezindua rasmi Kampeni ya
Upandaji Miti kandokando ya vyanzo vya maji nchi nzima mkoani Mtwara kwa lengo
la kuhakikisha vyanzo hivyo vinatunzwa na kuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo.
Profesa Mbarawa amezindua kampeni hiyo kwa kupanda miti nane katika
chanzo cha Mtawanya kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mjini na
kuzitaka Bodi zote za Mabonde tisa nchini kuweka mkazo na mipango madhubuti ya
kusimamia na kutunza rasilimali za maji ziweze kuwa endelevu.
Ametoa agizo hilo kutokana na uvamizi na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya
maji katika maeneo mengi kwa sasa nchini, hali inayohatarisha kiasi kikubwa cha
maji kupungua kutokana na vyanzo vingi kukauka, hali inayoweza
kusababisha ukosefu wa maji ya kutosha kwa ajili ya miradi inayoendelea
kutekelezwa na Serikali.
Na kutaka vyanzo vyote vya maji vitunzwe na kulindwa kwa kupandwa miti
maalumu inayohifadhi maji na kuagiza wale wote wanaofanya shughuli za
kibinadamu kwenye vyanzo waache tabia hiyo na watakao kaidi wachukuliwe hatua
kali ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa sheria inaweka bayana kuhusu jambo
hilo.
Ametoa tamko hilo kwa kuzingatia Sheria ya Maji Na, 11 ya Mwaka 2009
inayokataza kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji, na ikieleza
shughuli zote za kibinadamu zifanyike umbali wa mita 6o kutoka chanzo cha maji
kilipo na kutaka maeneo yote yawekewe mipaka na vizuizi kuonyesha ukomo wa watu
kuingia kwenye vyanzo hivyo.
‘‘Hatutaki kupata hasara kwenye miradi tunayowekeza fedha nyingi, halafu
baadae iwe kama magofu kwa kukosa maji. Imefika hatua kuwa ni lazima tuchukue
hatua za lazima kuinusuru taifa letu na uhaba wa maji.
Niwatake wananchi watoe
ushirikiano wa karibu na Serikali kuhakikisha vyanzo vyetu vyote vinakuwa
endelevu kwa kuzalisha maji ya kutosha na kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya
uhakika kwa miaka ijayo’’, amezungumza Profesa Mbarawa.
‘‘Kwa kuanza tumepanda miti nane katika chanzo hiki cha Mtawanya, nataka
ifikapo Disemba mwaku huu, nikute zaidi ya miti 1,000 kwenye chanzo hiki na
zoezi hili lifanyike nchi nzima kwa sababu kama waziri mwenye dhamana ya
kusimamia rasilimali za maji nitalisimamia jambo hili ipasavyo’’, ameonya
Profesa Mbarawa.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Evod Mmanda amesema ni muhimu zoezi la
upandaji miti liwe endelevu lenye kuzingatia upandaji wa miti na kuachana na
miti isiyo rafiki na maji kwa lengo la utunzaji wa maeneo yote yenye vyanzo na
kutaka wananchi wazingatie sheria iliyopo kwa hiari, pasipo kutumika nguvu na
kuonya kuwa hatavumilia uharibifu wa vyanzo vya maji katika wilaya yake.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Maji hivi karbuni imetoa Shilingi
Bilioni 2.3 kwa ajili ya malipo ya madai kwa wakandarasi mbalimbali
wanaotekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Mtwara, ambapo uzalishaji wa maji
kwa siku kwa mji wa Mtwara umefikia lita milioni 10, huku mahitaji kwa siku ni
lita milioni 13.7.
Fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo
ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma, ambapo hadi sasa miradi
45 ikiwa imeshakamilika na mingine 33 ikiwa katika hatua mbalimbali za
utekelezaji.
No comments:
Post a Comment