Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula akitoa maelekezo
kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rorya Charles Chacha mara baada ya
kumaliza kuzungumza na watendaji wa halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki.
.............................................
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumbà na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline
Mabula amepiga marufuku ugawaji viwanja ambavyo tayari vimemilikishwa huku
mmiliki wake wa awali akitafutiwa eneo lingine.
Hatua hiyo inafuatia kushamiri kwa tabia iliyozoeleka kwa baadhi ya
watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri mbalimbali hapa nchini kugawa
maeneo ambayo tayari yana wamiliki wake wa awali na kuwapa watu wengine wenye
uwezo kifedha huku wamiliki halali kuahidiwa kupatiwa kiwanja kingine.
Mhe. Mabula alitoa kauli hiyo wilayani Musoma mkoa wa Mara mwishoni mwa
wiki alipokutana na watendaji wa sekta ya ardhi katika Manispaa ya Musoma
pamoja na halmashauri za wilaya za Musoma na Butiama wakati wa ziara yake ya
kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya
februari mwaka 2018.
“Kuanzia sasa ni marufuku kwa watendaji wa sekta ya ardhi katika
halmashauri kugawa viwanja ‘pandikizi’ katika maeneo ambayo tayari
yameshamilikishwa kwa wananchi kwani suala hili limekuwa likileta migogoro
mikubwa katika sekta ya ardhi” alisema Mabula.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, suala
hilo limekuwa likijitokeza sana hasa maeneo yanayovutia na mara nyingi
linachangiwa na maafisa ardhi wasiokuwa waaminifu ambao humpatia mtu mwenye
uwezo kiwanja kilichomilikishwa kwa ahadi ya kumpatia mmiliki halali kiwanja
kingine.
Alisema, serikali ya awamu ya tano chini ya
Rais John Pombe Magufuli ambayo imekuwa ikiwatetea watu wa hali ya chini
haitavumilia hali hiyo iendelee kushamiri na kusema kuwa hatua kali
zitachukuliwa kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi watakaoendelea au kubainika
kufanya mchezo huo.
No comments:
Post a Comment