Monday, October 22, 2018

HALMASHAURI ZATAKIWA KUFANYA UTAFITI WA WAKANDARASI KABLA YA KUWAPA KAZI.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Sophia Kizigo (kulia) na wataalamu katika chanzo cha mradi wa Milonde, Namtumbo, mkoani Ruvuma.
.................................
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa ameziagiza Halmashauri zote kufanya utafiti wa kina kwa wakandarasi kabla ya kuingia nao mikataba ya ujenzi wa miradi ili kuweza kumaliza tatizo la utekelezaji mbovu wa miradi ya maji nchini.

Alisema tatizo la miradi mingi ya maji kwenye Halmashauri linatokana na kuwapa wakandarasi wasio na sifa, wengine wakishindwa hata na miradi midogo.

Waziri Mbarawa aliyasema hayo wakati akikagua miradi ya maji ya Kumbara-Litola, Milonje-Matemanga na Milonde katika Wilaya za Namtumbo na Tunduru, mkoani Ruvuma.

Profesa Mbarawa alisema Halmashauri nyingi zimekuwa zikitoa zabuni kwa wakandarasi katika mazingira ya rushwa, bila kuzingatia uwezo wao kifedha, vifaa vya kazi na kazi zao kwa sababu hawafanyi uchunguzi wa kina hivyo  kusababisha matatizo kwenye utekelezaji wa miradi.

Alisema Jambo la kutoa zabuni kusikozingatia sheria na taratibu kunapelekea kubadili wakandarasi na kuvunja mikataba mara mara kwa sababu ya utendaji mbovu wa wakandarasi, na kurudisha nyuma juhudi za Serikali kuwapatia wananchi wake huduma ya maji safi na salama.

“Serikali haitakubali kurudishwa nyuma kimaendeleo na mtu yeyote, tutawafukuza wakandarasi wasio na sifa na tutashughulika na wale wote wanaotoa zabuni pasipo kufuata utaratibu lazima niwaambie ukweli”, amesema Profesa Mbarawa.

“Ni lazima mfanye uchunguzi wa kina kwa kila mkandarasi kwa kuzingatia vigezo vyote, ikiwa ni pamoja na kwenda kuangalia kazi walizozifanya kwa lengo la kujiridhisha uwezo wake kabla hamjaingia nao mkataba”, ameonya Profesa Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa ameagiza Kampuni ya Service Plan Ltd isipewe tena kazi na wizara yake, baada ya kubainika imetoa taarifa ya usanifu wa mradi wa Kumbara-Litola isiyo sahahi uliopo Wilaya ya Namtumbo ambapo ungeigharimu Serikali fedha nyingi bila sababu.

Kulingana na usanifu wa awali kuonyesha gharama kubwa, ililazmika kufanya usanifu upya na kuonekana unaweza kutekelezwa kwa Shilingi Bilioni 1.2 baadala ya Shilingi Bilioni 6 kama ilivyoonyesha awali na mradi huo unategemewa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akikagua tenki la mradi wa Kumbara-Litola, Namtumbo na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Sophia Kizigo
Mradi wa maji Milonde ukiwa katika hatua ya utekelezaji.

No comments:

Post a Comment