Friday, October 19, 2018

RC. NDIKILO AZINDUA KAMPENI YA FURAHA YANGU KUPAMBANA NA VVU

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo akiwaonyesha wananchi  kadi mara baada ya kumaliza zoezi la kupima virisi vya ukimwi ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa kampeni ya furaha yangu yenye lengo la kupambana na maambukizi ya VVU, pamoja na kuwahimiza watu kupima afya zao.(PICHA NA VICTOR MASANGU)
................................

VICTOR MASANGU, PWANI 

KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kukabiliana na kupambana na  maambukizi mapya ya virusi vya vya ukimwi hatimaye Mkoa wa Pwani umezindua rasmi kampeni ijulikanayo  kwa jina la  furaha yangu kwa lengo la kuwahimiza wananchi wake kwenda kupima mapema ili kujua afya zao na kuanza kupatiwa matibabu endapo watabainika kuwa  na maambukizi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo akizungumza katika halfa hiyo ya  uzinduzi ambapo alikuwa mgeni rasmi  amebainisha kuwa lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuweka mipango ya kupambana na maambukizi mapya ya VVU  ambapo kwa sasa kiwango cha maambukizi  katika ngazi ya Mkoa kimepungua kutoka asilimia 7.1 kwa mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 5.5 kwa mwaka wa 2017.

“Kampeni hii inawalenga watanzania wote watambue hali zao za maaambukizi ya VVU.hususan kwa wanaume na makundi mengine ambayo ni wasichana walio katika umri wa balehe, wanawake na vijana wenye umri wa miakaa 15-24 akinammama wajawazito na wanaonyonyesha  sambamba na watoto wao,”alisema Ndikilo.

Aidha Ndikilo alibainisha kuwa hali ya wananchi kutokujua hali zao za maambukizi ya virusi vya ukimwi katika Mkoa wa Pwani inaweza kuleta atharu kubwa kwa wenza na familio zao na pia inadhoofisha mapambano dhidi ya ukimwi hivyo amewaasa wananachi wote kujenga tabia ya kupima  kwa lengo la kuweza kujua afya zao. 

Kwa upande wake Kaimu mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hussein Athumani alisema  kwamba lengo lao ni kuhakikisha wanaweka mipango ya kuwaelimisha wananchi katika maeneo mbali mbali ili kuweza kupunguza kasi ya maambukizi mapya  ya virusi vya ukimwi pamoja na kuongeza vituo vingine  kwa ajili ya utoaji wa dawa za kufubaza.

Nao baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Pwani ambao wamehudhuria katika uzinduzi huo wanaoishi na na maambukizi ya VVU akiwemo Bahatisha Hemed na Ibrahimu Venasi hawakusita kutoa ushuhuda wao huku wakiitaka jamii kuachana na vitendo vya kuwanyanyapaa  na badala yake wawashirikishe kikamilifu  katika shuguli mbali mbali za kimaendeleo.

UZINDUZI wa kampeni ya furaha yangu katika Mkoa wa Pwani utaweza kuleta mkombozi mkubwa kwa wananchi kutokana na  mikakati ambayo imepangwa kwa ajili ya kutoa mafunzo na elimu ambayo itawasaidia na kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi huku kauli  mbiu  yake ikisema kwamba Pima ,jitambue, na Ishi

 

No comments:

Post a Comment