Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh
Hasani Bin Mussa Kabeke wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa
Mwanza Oktoba 22, 2018 akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako
kesho anatarajia kufungua maonesho ya wajasiriamali.
Sheikh huyo
amechaguliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, John Mongella.
..............................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ushirikiano mzuri baina ya
taasisi mbalimbali za dini nchini na Serikali ni jambo la muhimu katika
kuboresha na kuimarisha amani.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 22, 2018) alipowasili jijini Mwanza
akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako kesho anatarajia kufungua maonesho ya
wajasiriamali.
Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, Waziri Mkuu amepokelewa na
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na viongozi mbalimbali wa mkoa huo
wakiwemo wa Serikali na wa dini mbalimbali.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mkakati wa viongozi wa dini wa
kuunda kamati za amani nchini ambapo walianzia kwenye ngazi ya mkoa na sasa
wamefikia katika kata.
“Viongozi wa dini mnadhamana kubwa katika kulifanya Taifa
liendelee kudumisha amani, utulivu na mshikamano, hivyo ushirikiano wenu
na Serikali ni muhimu.”
Amesema viongozi wa Serikali wakati wote wamekuwa tayari kufanyakazi na
viongozi pamoja na taasisi mbalimbali za dini, lengo ni kuimarisha amani na
utulivu uliopo nchini.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Mwanza inawajibu wa kuhakikisha kwamba maeneo ya mkoa huu yanaendelea kuwa
salama.
Pia, Waziri Mkuu amempongeza Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan
Bin Mussa Kabeke kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.
“Nakupongeza kaimu sheikh wa mkoa kwa kuteuliwa na ninakutakia kila la
heri katika kazi yako na kwamba dhamana yako kubwa ni kuwaunganisha waislamu na
waumini wa dini zote.”
No comments:
Post a Comment