Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza
na wananchi wenye migogoro ya ardhi katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na
Halmashauri ya Moshi Vijijini mkoa wa Kilimanjaro alipoenda kuonana na Lukuvi
katika program ya Funguka kwa Waziri.
.......................................
Na Munir Shemweta, WANMM Kilimanjaro
Waziri wa Ardhi Nyumba na Mandeleo ya Makazi William
Lukuvi amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kujisahihisha ili kuepusha
mogogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwaumuzi wananchi wengi.
Lukuvi alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wananchi
97 wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Moshi Vijijini katika
mkoa wa Kilimanjaro waliojitokeza kwa ajili ya kuwasilisha kero zao za ardhi
kupitia program ya Funguka kwa Waziri.
Alisema, ni vyema katika kipindi hiki cha Serikali
ya awamu ya tano watendaji wa sekta ya ardhi wakaanza kujisahihisha ikiwemo
kuweka majalada yote ya ardhi vizuri kabla hajatembelea maeneo yao kinyume
chake atawashughulikia wote watakaobainika kukaidi ama kutoweka sawa majalada
ya ardhi.
“Mtu yeyote anayetaka kuingusha Serikali katika
masuala ya ardhi tutamuangusha yeye na lazima tutekeleze ilani ya Chama cha
Mapinduzi kwa vitendo” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Serikali itawanyoosha wale wote wanaoenda kinyume na maadili ya
utumishi na kubainisha kuwa hata wale watendaji wa ardhi walioharibu huko nyuma
watashughulikiwa.
Akigeukia migogoro ya ardhi, Lukuvi alisema migogoro
mingi inayojitokeza sasa ni ile ya miaka ya nyuma ya kuanzia miaka ya themanini
na kubainisha kuwa kupungua kwa migogoro mipya kunatokana na Serikali ya sasa
kuweka mazingira mazuri ya kushughulikia masuala ya ardhi.
“Leo watendaji wa sekta ya ardhi wamenyooka na kazi
ya serikali ya awamu ya tano ni kuwanyoosha wale wanaoenda kinyume na taratibu
na sheria katika kushughulikia masuala ya ardhi.
Akigeukia suala la wamiliki wa ardhi kuchukuliwa
maeneo yao bila kulipwa fidia, Lukuvi amewahakikishia wananchi waliohudhuria
mkutano huo kuwa, Serikali inalipa kipaumbele suala la fidia kwa wale ambao
maeneo yao yatachukuliwa.
Aliwaeleza kuwa hata ikitokea mtu hakufidiwa kipindi
ambacho eneo lake limechukuliwa lakini malipo yake yataanza kuhesebiwa pale
eneo lilipochukuliwa na kiwango cha fidia kitakuwa kikiongezeka kadiri malipo
yake yanavyochelewa.
Pia aliwaeleza wananchi waliokusanyika katika ukumbi
wa ofisi wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa wale wote ambao maeneo yao yalishatolewa
maamuzi na Mahakama hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kubatilisha ikiwemo
Serikali.
Sehemu ya wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Moshi na Halmashauri ya Moshi Vijijini waliojitokeza kumuona Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kwa ajili ya kuwasilisha migogoro
ya ardhi katika program ya Funguka kwa Waziri. (Picha zote na Wizara ya Ardhi)
No comments:
Post a Comment