Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes
Kijazi (kulia) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa
uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu
kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua, kipindi cha miezi ya Novemba, 2018
hadi Aprili, 2019, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa
Utabiri, Samwel Mbuya akifuatilia.
.......................................
MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa uchambuzi wa mwenendo wa
mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu
mmoja wa mvua, katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2018 hadi Aprili, 2019.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa
TMA, Dk. Agnes Kijazi amesema Mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi
wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Njombe,
Iringa, Ruvuma, kusini mwa mkoa wa Morogoro, Lindi na Mtwara.
Alisema maeneo ya mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe yanatarajiwa
kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, huku vipindi vingi vya mvua
vikitarajiwa nusu ya kwanza ya msimu wa Novemba, Desemba, Januari, Februari,
Machi na Aprili, 2018/19 na kupungua nusu ya pili ya msimu huo.
“Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi
Novemba, 2018 katika mikoa ya Kigoma na Katavi na wiki ya tatu na ya nne katika
maeneo mengine yaliyosalia. Mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya
mwezi Aprili, 2019 katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua,” alisema
Dk. Kijazi.
Aidha, kutokana na mvua za vuli katika maeneo hayo ametoa ushauri na
tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa
katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula,
Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na
Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa.
Aliongeza kuwa mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu
mmoja wa mvua kwa mwaka Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Wanyamapori Katika kipindi cha
mvua za ‘Msimu’ (Novemba hadi Aprili) 2018/19, hali ya unyevunyevu wa udongo
kwa ustawi wa mazao na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika
katika maeneo mengi.
Hata hivyo, alibainisha kuwa mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile
mahindi, maharage na mtama, yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa
kupitiliza na maji kutuama.
“…Magonjwa ya wanyama na uharibifu wa miundombinu ya kilimo na ile ya
kufugia samaki vinaweza kujitokeza kutokana na mvua za juu ya wastani
zinazotarajiwa katika maeneo hayo. Kwa upande mwingine, malisho na upatikanaji
wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha
katika maeneo mengi,” aalisisitiza katika taarifa yake.
No comments:
Post a Comment