Tuesday, October 16, 2018

TAMASHA LA SANAA BAGAMOYO WANANCHI WAKARIBISHWA.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbart Makoye ametoa wito  kwa wakazi wa Bagamoyo na nchi nzima kuhuduria Tamasha la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linalotarajiwa kuanza Tarehe 20 Oktoba 2018.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Chuo hicho Dkt. Makoye alisema kuhudhuria Tamasha hilo ni fursa kwa watanzania na wale wa nje ya Tanzania kujionea taaluma mbalimbali zinazofundishwa chuoni hapo.

Alisema chuo hicho ambacho ni kikongwe hapa nchini kwa kutoa taaluma za sanaa na utamaduni kinawapa fursa vijana kujiajiri katika fani wanazopata chuoni hapo.

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa, Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo hufanyika kila mwaka na kuandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) likiwa na malengo ya

>Kutunza na kuenzi sanaa na utamaduni wa Mtanzania.

>Kutengeneza jukwaa ambalo wanafunzi wa TaSUBa wanalitumia kupima kiwango chao cha umahiri katika sanaa kwa mwaka katika fani za sanaa za maonyesho na zile za ufundi.

>Kukutanisha watu wa tamaduni mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali Duniani ili kuonyesha utajiri wao wa sanaa na utamaduni.

>Kutengeneza jukwaa ambalo ni kiungo cha kujenga mahusiano ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kupitia maonyesho ya sanaa na pia kubadilishana uzoefu na mawazo katika kuendeleza tasnia ya  ya sanaa.

Dkt. Makoye alisema mwaka huu Tamasha linafanyika kwa mara ya 37 na litapambwa na mambo mbalimbali ikiwemo Sarakasi, maigizo pamoja na maonyesho ya sanaa za ufundi.

Aidha, alisema katika Tamsha hilo kutakuwa na warsha na semina zitakazohusu mambo mbalimbali ya kijamii.

Jumla ya vikundi vya sanaa 100 vimethibitisha kushiriki na kati ya hivyo vikundi 10 ni kutoka nje ya nchi ambazo ni Kenya, Uganda, Zimbabwe, Ivory Coast, Ufaransa, Zambia,Cameroon, Ujerumani na Finland.

Aliongeza kwa kusema kuwa, ufunguzi rasmi  wa Tamasha hilo utafanyika Tarehe 20 Oktoba 2018 ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Dkt. Harrison Mwakyembe na litafungwa Tarehe 27 Oktoba 2018  ambapo mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Juliana Shonza.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni Sanaa na Utamaduni katika kukuza Uzalendo.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbart Makoye akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Chuo hicho Mjini Bagamoyo leo Tarehe 16 Oktoba 2018.
  
Baadhi ya wakufunzi na wageni kutoka nje ya nchi wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Dkt. Herbert Makoye alipokuwa akizzungumza katika ukumbi wa TaSUBa, Bagamoyo.

No comments:

Post a Comment