Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata
maelezo kutoka kwa Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Masanja Kadogosamara baada ya kutembelea banda la
kampuni inayotengeneza reli mpya ya kisasa ya YAPI MERKEZ wakati wa ufunguzi wa maonyesho
ya wiki ya Viwanda mkoani Pwani. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
..............................................
NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA.
MAKAMU wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu amewaasa
watanzania kujenga utamaduni wa kununua bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda
vya ndani pamoja na wawekezaji kununua malighafi za viwanda vilivyopo
nchini .
Aidha ametoa rai kwa wadau na taasisi zote zinazosimamia miundombinu
wezeshi ,uzalishaji na huduma ,kuweka mkakati madhubuti ambayo inaweza kuweka
mazingira wezeshi kwa ustawi wa viwanda .
Samia aliyasema hayo wakati akifungua maonyesho ya bidhaa zinazozalishwa
na viwanda vya mkoa wa Pwani ambayo yatafungwa Novemba 4 mwaka huu .
Pamoja na hayo ,ameuelekeza mkoa wa Pwani kutumia wawekezaji kuboresha
chuo cha ufundi cha Kongowe ili wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo ya
kidato cha tano waweze kwenda kupata ujuzi na baadae wapate ajira kirahisi
viwandani .
Samia alisema ,watanzania na wawekezaji wa ndani wamekuwa hawana kasumba
ya kununua vya kwao ambapo wamekuwa wakikimbilia bidhaa zinazotoka nje ya nchi
.
Alieleza ,taswira ya uchumi wa viwanda wa viwanda inahusisha mnyororo
mzima kuanzia uzalishaji ,utunzaji na usafirishaji wa malighafi kutoka kwenye
maeneo ya uzalishaji hadi viwandani ,uchakataji usindikaji ,ufungishaji
wa bidhaa na usafirishaji wake kutoka viwandani hadi kwa walaji.
Samia alisema ,ili mnyororo huo ufanikiwe inahitaji miundombinu wezeshi
na saidizi kama vile umeme,maji ,barabara na mawasiliano pia raslimali ,mifumo
ya kitaasisi ,sheria na huduma za kifedha.
“Katika kulijua hili serikali kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo
TRL,Dawasa na Tanesco sasa zinajielekeza nguvu katika mkoa wa Pwani kuhakikisha
umeme,maji ,miundombinu inakuwa ya uhakika ,ili mnyororo wa uchumi wa viwanda
uwe vizuri zaidi”alisema Samia.
Kuhusu vijana aliwahimiza kusoma ili kupata ujuzi kwa lengo la kuajiriwa
kuliko kutegemea kazi za vibarua.
Alizitaka sekta zinazoshughulikia maslahi ya wafanyakazi wazunguke kuona
jinsi wafanyakazi wanavyohudumiwa.
” Wafanyajazi wengine wana wanafanyakazi za uzalishaji bila kupumzika
huko viwandani ,masaa ya kazi yanajulikana ,hivyo haki na maslahi yao
yapatikane “alifafanua Samia.
Nae waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji ,Charles Mwijage alisema
Tanzania inajenga uchumi wa Kitaifa ,ifikapo 2020-2025 wastani wa kipato cha
mtanzania iwe milioni 7.5 kwa mwaka.
Aliupongeza mkoa wa Pwani kwa kutoa ajira za moja kwa moja 20,000
kwa kipindi cha miaka mitatu.
“Ukitaka soka nenda Brazil ,ukitaka viwanda nenda Pwani “alisema Mwijage.
Mwijage alisema kuwa, Tanzania inatumia saruji tani milioni 4.8 kwa mwaka
alimhakikishia Samia kwasasa wanauwezo wa kutengeneza saruji milioni 10.8
,wanauwezo mkubwa kuzidi mahitaji.
Awali mkuu wa mkoa huo ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema makamu wa Rais
alikuwa mkoani hapo kwa siku tano ziara ambayo imeleta tija kwa wana Pwani.
Alisema maonyesho hayo yataweza kufungua soko zaidi kwa viwanda kwa
kujitangaza.
Ndikilo alisema mkoa una jumla ya viwanda 429 ambapo vikubwa na vya kati
109, vidogo 320 na vya kusindika vipo 86.
Alitaja changamoto inayozikabili baadhi ya viwanda kukosa soko la uhakika
hali inayosababisha kusuasua kwa uzalishaji.
No comments:
Post a Comment