Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua
utandikaji wa Reli ya SGR katika eneo la Soga mkoani Pwani, Oktoba 3,
2018. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi,
Isack Kamwelwe.
...............................................
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema
ameridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa mfumo wa reli ya kisasa (SGR)
inayojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi.
Amesema kipande cha kutoka Dar es
Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa km. 300 ambacho kilitakiwa kukamilika
Julai 2019, wataalamu wamesema watakamilisha Aprili 2019.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi,
Novemba 3, 2018) alipotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia eneo
la Shaurimoyo Dar esSalaam hadi Soga, Pwani.
“Nimeridhishwa na viwango na
maendeleo ya ujenzi kwa sehemu ulivyofikia pamoja na ushiriki wa Watanzania
wengi katika mradi huu, tunataka muendelee kujenga kwa kasi hii.”
Waziri Mkuu amesema Serikali inataka
kuona malengo ya Rais Dkt. John Magufuli ya kutaka kuona
SGR inakamilika na kuanza kutumika nchini yanatimia.
Kuhusu suala la ajira, Waziri Mkuu
amesema amefarijika kusikia asilimia 96 ya watu walioajiriwa katika mradi huo
ni Watanzania, amewataka wawe mabalozi wazuri.
“Watanzania mnaofanya kazi katika
mradi huu hakikisheni mnawajibika kwa kufanyakazi kwa bidii, uaminifu na muwe
mabalozi wazuri ili wengine waweze wapate ajira.”
Awali,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema awamu ya kwanza ya mradi huo wa
reli kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora unagharimu sh. trilioni
7.1.
Alisema mradi wa ujenzi wa reli hiyo
yenye urefu wa km 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza umegawanyika katika
vipande vitano, kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye
urefu km 300 na kitagharimu sh. trilioni 2.7.
“Kipande kingine ni kutoka Morogoro
hadi Makutupora chenye urefu wa km. 422 ambacho kitagharimu sh. trilioni 4.4,
Makutupora hadi Tabora km. 376.5, Tabora hadi Isaka km 162.5 na Isaka hadi
Mwanza km. 311.25.”
Mkurugenzi huyo alisema kukamilika
kwa reli hiyo ya kisasa kutachochea mipango ya Serikali katika kutekeleza sera
ya viwanda na kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Pia reli hiyo itachochea mapinduzi ya
kiuchumi kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati hususan kwa nchi
zisizopakana na bahari kwani watasafirisha mizigo yao kwa haraka na uhakika.
Akizungumzia mradi huo kwa ujumla,
Kadogosa alisema maendeleo ya mradi huo ni asilimia 32 kwa kipande cha Dar es
Salaam-Morogoro na asilimia 3. 31 kwa kipande cha Morogoro-Makutupora.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua
utandikaji wa Reli ya kisasa ya SGR katika eneo la Soga mkoani
Pwani, Oktoba 3, 2018. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe na kulia kwa Waziri Mkuu ni Mkurugenzi
Mkuu wa Shiraki la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa
No comments:
Post a Comment