WATU saba ambao majina yao
hayajafahamika mara moja wamefariki dunia na watatu kujeruhiwa katika ajali
iliyohusisha magari mawili ya serikali na lori moja, majira ya saa 6:30 usiku
wa kuamkia leo Jumamosi, Novemba 3, 2018 katika Kijiji cha Mbande, Kata ya Sejeli,
Tarafa na Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Katika ajali hiyo, gari lenye namba
za usajili STL 6250 Toyota Land Cruiser mali ya ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) ikiendeshwa na Dickson Kitanda (42) Mgita, mkazi wa Dar es
Salaam ikitokea Dodoma kuelekea Dar ikiwa na abiria sita iliigonga kwa nyuma
gari namba T161 CBB/T152 CBB lori aina ya DAF mali ya Z.S Ally mkazi wa Dar
iliyokuwa imeharibika barabarani.
Inaelezwa kuwa, baada ya ajali
hiyo, STL 6250 iligongana uso kwa uso na gari lingine SU 41173 Toyota Land
Cruiser mali ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (PSSSF) ikitokea Dar
kuelekea Dodoma ikiendeshwa na Peter Elleson Masamu (35) Mchaga mkazi wa Dodoma
ikiwa na abiria watatu ambao ni Elliad Eliyakunda Mdeme (40), Mwanasheria na
mkazi wa Dodoma, Vick Elisala Moshi (51) Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi
Mkuu wa PSSSF na Abubakar Mjata Ndwaqta (42) Ofisa Takwimu wa PSSSF mkazi wa
Kisasa, Dodoma.
Taarifa za awali zinasema waliofariki
kwenye ajali hiyo iliyotokea katika Barabara Kuu ya Dodoma – Morogoro, ni
ndugu sita wa Naibu CAG waliokuwa wakitoka kwenye msiba Chato mkoani Geita,
kati yao wanawake wawili ambao ni abiria wa gari STL 6250 T/ Land Cruiser na
dereva wa gari hilo la ofisi ya CAG huku majeruhi wakiwa watatu, abiria wa gari
SU 41173 T/Land Cruiser.
Miili ya marehemu imepelekwa
Hospitali ya Kongwa na majeruhi watatu wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma. Chanzo cha ajali bado kinachunguzwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
RPC Gilles Muroto amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment