Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbas
Na Grace Semfuko-MAELEZO
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbas amesema Serikali ya awamu
ya tano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli imeongeza kasi ya ujenzi wa
Hospitali za Wilaya na vituo vya afya nchini ambapo kwa miaka mitatu
pekee jumla ya vituo hivyo 67 vimejengwa ukilinganisha na 77 vilivyojengwa
miaka 53 iliyopita tangu uhuru.
Dkt Abbasi amesema hatua hiyo ya Serikali ya ujenzi wa kasi wa hospitali
na vituo vya afya inalenga kuimarisha afya za watanzania ambapo hivi sasa idadi
kubwa ya watanzania inatumia huduma za bima ya afya ya Taifa NHIF idadi ambayo
awali ilikuwa milioni 9.9 mwaka 2015 mpaka kufikia zaidi ya milioni 16 Mwaka
huu wa 2018.
Akizungumza nkatika semina ya Waandishi wa Klabu ya waandishi wa Habari
wa Mkoa wa Dar Es Salaam (DDCPC) iliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya NHIF iliyokuwa na lengo la kujengeana uwezo ili umma wa watanzania waweze
kunufaika zaidi katika huduma za Afya Nchini, Dkt Abbasi amesema ipo haja kwa
waandishi wa habari hao kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano
ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.
“Unajua hata sisi waandishi wa habari tunayo haki ya kupongeza,pale
unapoandika changamoto na zikafanyiwa kazi ni muhimu kupongeza pia sio kukosoa
tu, juhudi za Serikali ya awamu ya tano kwa kipindi kifupi tu makubwa yamefanyika
ukilinganisha na kipindi kingine chochote” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji
Mkuu wa Serikali.
Aidha Dkt Abbasi amewataka waandishi wa Habari Nchini kutumia kalamu zao
katika kuandika mafanikio makubwa ya miaka mitatu yanayofanywa na rais
Dkt John Pombe Magufuli.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma za wanachama wa Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya NHIF Bw. Mbarouk Magawa amesema idadi hiyo ya wanachama
iliyoongezeka inaufanya mfuko huo kuzidi kujiimarisha na kuhudumia wanachama
wengi zaidi.
Mbarouk amesema kuongezeka kwa idadi hiyo ya wanachama kunaifanya
Juhudi za Serikali ya awamu ya tano kufikia malengo yake ya kuhakikisha
huduma za afya nafuu zinapatikana nchini kote.
“Mfuko wa Taifa wa Bima za Afya lengo letu ni kuhudumia wanachama wengi
zaidi na kwa awamu hii chini Uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli wanachama
wengi zaidi wameongezeka tangu kuanzishwa kwa mfuko huu mwaka 2001” alisema
Magawa Mkurugenzi wa Huduma za wanachama wa NHIF.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya ulianzishwa kwa Sheria namba 8 ya Bunge ya
mwaka 1999 na mfuko huo ulianza kufanyakazi rasmi mwaka 2001,hadi sasa
mfuko huo una wanachama zaidi ya milioni 16 kutoka Milioni 9.9 waliokuwepo hapo
awali.
No comments:
Post a Comment