WAZIRI wa Nishati Dkt Medard Kaleman
Na Grace Semfuko-MAELEZO
WAZIRI wa Nishati Dkt Medard Kaleman, ameuagiza uongozi wa Serikali ya
Mkoa wa Pwani kuainisha maeneo yote kwa uwekezaji wa viwanda ili kuharakisha
miundo mbinu ya nishati ya umeme utakaosaidia kuhamasisha wawekezaji na hivyo
kusaidia kukuza uwekezaji wa viwanda.
Dkt. Kalemani ameyasema hayo alipotembelea maonesho ya bidhaa za
viwandani katika Viwanja vya Sabasaba vilivyopo Picha ya Ndege, Wilaya ya
Kibaha Mkoani Pwani, akasisitiza kuwa wakati Serikali ya awamu ya tano
inaweka mikakati ya kuhakikisha kunakuwa na viwanda vya kutosha kuinua uchumi
wa Taifa watendaji wa Serikali hiyo hawana budi kuimarisha miundombinu yake na
kupanua fursa.
“Mkoa wenu huu wa Pwani ni Mkubwa na wenye ardhi na rasilimali za kutosha
kabisa, ainisheni maeneo ya uwekezaji na mtuambie tuje kuweka miundombinu ya
nishati, sisi tutafanya kazi hiyo haraka, kwani tunataka uwekezaji uwe mkubwa
ili Nchi yetu iweze kupata manufaa makubwa kiuchumi” alisema Dkt. Kalemani.
Pia Waziri Dkt Kalemani amewataka wawekezaji nchini kuongeza bidii katika
kujenga viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ili kuwawezesha Watanzania
kupata ajira pamoja na kuiingizia Serikali pato kutokana na kodi mbalimbali za
uuzwaji wa bidhaa hizo.
Waziri huyo pia ametoa wito kwa viongozi wa mikoa mbalimbali nchini
kutenga maeneo ya uwekezaji ili kuwawezesha wawekezaji kutoka katika mataifa
mengine kuja kuwekeza bila kuwa na vikwazo vya kiuchumi.
Pia Waziri Kalemani amesema katika kukabilina na changamoto za
miundo mbinu ya nguzo za miti kwa ajili ya Umeme kuharibika hususani katika
maeneo yenye maji mengi amewataka wadau wanaotengeneza nguzo za umeme za zege
kuboresha bidhaa hiyo ili ziweze kuingia katika ushindani na hatumaye ziweze kupata
masoko zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amesema Mkoa wake unafanya
kila jituhada za kuhakikisha miundombinu rahizi inafikika kwenye maeneo
yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda na kuwaagiza watendaji katika Halmashauri
zote kutenga maeneo ya uwekezaji.
“ Sisi Mkoa wa Pwani tunayo maeneo ya kutosha kabisa katika uwekezaji, na
tunafanya kila jitihada za kuhakikisha miundombinu rahisi ikiwepo ya
Barabara,Maji na Umeme inafikika ili viwanda vijengwe na vianze uzalishaji wa
bidhaa mara moja” alisema Mhandisi Ndikilo.
Nae Meneja wa kiwanda kinachotengeenza nguzo za umeme za zege cha
East Africa Infrastructure Engineering Limited, JohnsPeter Majura
amesema wameanza kuzalisha nguzo za umeme ili kuimarisha miundombinu ya umeme
kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Asumpta Mshama amesema Wilaya yake tayari
imeanza kuvutia wawekezaji kwa kutenga maeneo ya uwekezaji ambayo tayari
yameanza kupata wawekezaji kutoka katika mataifa mbalimbali duniani.
Maonesho ya bidhaa za viwandani katika Mkoa wa Pwani yalifunguliwa
tare 29 ili kutangaza bidhaa mbalimbali za uwekezaji katika mkoa huo na
yatafungwa Nov. 3, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment