WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine
Shigela orodha ya matrafiki wanaodaiwa kuwaomba rushwa madereva wa noah
wilayani Lushoto.
Majina ya trafiki hao wanadaiwa kuomba rushwa kwa madereva wa noah
wanaofanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya wilaya hiyo yaliwasilishwa kwa
Waziri Mkuu kupitia mabango.
Waziri Mkuu alimkabidhi majina hayo jana jioni (Jumatano, Oktoba 31,
2018) baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Sabasaba,
Lushoto mjini.
Baada ya kumkabidhi majina hayo alimuagiza afanye uchunguzi wa tuhuma za
rushwa zinazowakabili askari hao na kisha awasilishe taarifa kwake leo Alhamisi
Novemba 1, 2018.
Mbali ya wananchi kuwasilisha malalamiko hayo, Pia mbunge wa Lushoto,
Shaaban Shekilindi alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua kero hiyo inayowakabili
wananchi.
Awali, Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya
Lushoto katika ukumbi wa chuo cha Mahakama Lushoto ambapo aliwasisitiza wafanye
kazi kwa bidii.
Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli
haina msamaha na mtumishi wa umma asiyetaka kufanya kazi kwa bidii na
kuzingatia weledi.
Alisema watumishi wa umma wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya
utumishi ili waweze kutimiza lengo la Serikali la kuwahudumia wananchi kwa
kutumia taaluma zao.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi
mkoani Tanga alisema Serikali haina msamaha na mtumishi asietaka kubadilika na
kufanya kazi.
Pia, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma wahakikishe fedha
zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo
zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka Wakuu wa Idara kutumia kitabu cha ilani
ya uchaguzi cha CCM cha mwaka 2015/2020 kwa sababu kina maelekezo wanayopaswa
kuyatekeleza.
“Kitabu kile kina maelezo ya msingi yaliyotolewa na Rais. Dkt. Magufuli
ambayo yanatakiwa yapewe kipaumbele cha utekelezwaji, wakuu wa Idara ni muhimu
musome na kutekeleza.”
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa wilaya wahakikishe
wanasimamia utekelezwaji wa maelekezo yote yaliyoainishwa kwenye kitabu cha
Ilani katika maeneo yao.
Kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali nchini,
Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na kwamba suala hilo linaendelea
kufanyiwa kazi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba na kuwapongeza wakazi hao kwa
kutunza misitu.
Alisema maeneo mengi nchini wananchi wamekata miti na kusababisha kukauka
kwa vyanzo vya maji, ambapo ni tofauti na wilaya ya Lushoto ambayo bado ina
misitu minene.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wote wa vijiji na
kata waainishe sehemu zote zenye misitu na vyanzo vya maji katika
maeneo yao na wahakikishe wanayalinda.
Alisema mtu yeyote atakayebainika kuharibu mazingira hayo iwe kwa kuchoma
au kukata miti achukulie hatua kali. “Ni marufuku mtu yeyote kukata miti bila
kibali cha Serikali.”
Nae, Mbunge wa Lushoto Shekilindi alimuomba Waziri Mkuu awasaidie
katika kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa katika
jimbo hilo ikiwemo ya afya.
Mbunge alisema kwa sasa hospitali ya wilaya hiyo inakabiliwa na ukosefu
wa mashine ya x rey, hivyo kusababisha wananchi kusafiri hadi Korogwe au Tanga kufuata
huduama hiyo.
Waziri Mkuu alisema tayari ameshamuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kupeleka mashine ya x-rey katika
hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment