WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema amefarijika na maendeleo ya ujenzi wa
viwanda kwenye mkoa wa Tanga kwa sababu vitasaidia katika ukuaji wa uchumi na
kuongeza ajira.
Aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Novemba 1, 2018) alipotembelea
kiwanda cha saruji cha Rhino na kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh, vyote vya
jijini Tanga.
Waziri Mkuu ambaye jana alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu
mkoani Tanga, aliwapongeza wawekezaji wa viwanda hivyo kwa kuunga mkono mkakati
wa Serikali.
Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli imedhamiria kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati ifikapo 2025
kwa kupitia sekta ya viwanda.
Akizungumzia kuhusu kiwanda cha Rhino, Waziri Mkuu alisema kiwanda hicho
na vingine vya saruji nchini vitasadia kupunguza gharama ya saruji nchini na
kurahisisha ujenzi.
“Serikali inaamini kwamba uwepo wa viwanda mbalimbali nchini si tu
utawezesha ukuaji wa uchumi wa Taifa, pia utasaidia katika kumaliza changamoto
ya ajira hususani kwa vijana.”
Akiwa katika kiwanda cha Tanga Fresh, Waziri Mkuu aliwataka wafugaji
mkoani Tanga wabadili mfumo wa ufugaji na wafuge kwa kutumia njia za kisasa ili
waongeze uzalishaji.
“Wafugaji lazima wakubali kubadilika watumie fursa ya uwepo wa kiwanda
hiki kwa kufuga kisasa ili wapate maziwa mengi kwa sababu wana uhakika wa
kuyauza kiwandani hapa”.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka wananchi walioajiriwa kiwandani hapo
wafanye kazi kwa bidii, uaminifu na wawe waadilifu na wasijihusishe na vitendo
vya wizi kwa kuwa havina tija.
No comments:
Post a Comment