Thursday, November 1, 2018

SAYONA FRUITS YAKABIDHI MAJENGO YA MILIONI 70 PAMOJA NA VIFAA TIBA KWA HALMASHAURI YA CHALINZE

Msaidizi wa Mkurugenzi  Mtendaji wa Sayona Bw Aboubakary Mlawa (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Bi Amina Kiwanuka, majengo pamoja vifaatiba vyenye thamani ya shilingi milioni 70 katika Zahanati ya Msoga.
...................................
 
Kampuni ya Sayona Fruits Limited ya  mboga Chalinze mkoani Pwani imekabidhi majengo na vifaa tiba yaliyogharimu shilingi milioni 70 kwa zahanati ya Kijiji cha Mboga.

Akikabidhi msaada huo,kwa Mkurungezi Mtendaji wa Halmashauri ya Bibi Amina  Kiwanuka, Msaidizi wa Mkurugenzi  Mtendaji wa Sayona Bw Aboubakary Mlawa alisema jumla ya shilingi milioni sabini zimetumika.

Alisema licha ya kusaidia sekta mbalimbali kijijini hapo ambapo ndipo kilipo kiwanda cha Sayona,wameamua kujenga nyumba ya mganga,jengo lenye maabara, mapumziko  na    duka la dawa.

Bw Mlawa alisema kutokana na ushirikiano mzuri baina ya kiwanda na jamii wameona ni muhimu kuboresha zahanati hiyo ambayo pia inasaidia kutoa huduma kwa wafanyakazi kwa kushirikiana na zahanati iliyopo ndani  ya kiwanda.

Aliongeza kuwa pamoja na kuboresha huduma pia kiwanda kitasaidia usafiri wa gari la wagonjwa pale itakapohitajika kupeleka hospitali kubwa kutokana na kuwepo gari la wagonjwa kiwandani.

Akishukuru kwa msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Bibi Amina Kiwanuka alisema msaada huo wa Sayona umekuja wakati muafaka kwani mikakati ya Halmashauri ni kuboresha sekta ya afya katika Kijiji vyote.
Alisema Sayona ni moja ya kampuni ambayo ni mdau mkubwa wa maendeleo wilayani Bagamoyo,hivyo ushirikiano wake unampa faraja hata katika shughuli zake katika Halmashauri ya Chalinze.

Bibi Kiwanuka amewataka watumishi wa zahanati  hiyo kuhakikisha majengo na vifaa vinatunzwa na kulindwa.

Sayona Fruits Limited inamiliki kiwanda cha kusindika matunda na kuzalisha juisi za aina mbalimbali.
 
Msaidizi wa Mkurugenzi  Mtendaji wa Sayona Bw Aboubakary Mlawa akiwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai pamoja watumishi wengine wakati wa kukabidhi majengo na vifaatiba vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 70 katika Zahanati ya Mboga.

Muonekano wa majengo hayo ya Zahanati ya Mboga ambayo yamejengwa na Kampuni ya Sayona Fruits yaliyogharimu shilingi milioni 70 pamoja na vifaatiba.

No comments:

Post a Comment