Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
amewa himiza watanzania kushirikiana na Serikali yake katika masuala makubwa ya
msingi ili kuliletea Taifa maendeleo ya haraka.
Akizungumza leo katika ukumbi wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es
salaam, wakati wa Kongamano kuhusu hali ya uchumi na Siasa nchini, lenye
mada isemayo “Miaka Mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano Tunatoka Wapi, Tuko
Wapi na Tunakwenda Wapi?”, Rais Magufuli alisema kuwa anawaomba watanzania
kuendelea kushirikiana Serikali yake ili kujiletea maendeleoa.
“Nawaomba watanzania katika mambo makubwa ya msingi ni lazima tusimame
kwa pamoja, na si kujali itikadi za vyama vyetu vya siasa”alisema Rais Magufuli.
Aidha, alisisitiza kuwa “ mambo ya chama yatatuchelewesha, watanzania
hawataki vyama, wanataka maendeleo”
Katika kongamano hilo ambalo Rais Magufuli alikuwa mgeni maalum,
amesisitiza namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwaletea
maendeleo watanzania kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kujenga uchumi.
Rais Magufuli amekaribisha sekta binafsi katika kilimo ili kuimarisha
sekta hiyo kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa na ikiwa ni pamoja na kupata
soko la uhakika la mazao ya wakulima.
“Benki ya kilimo ina shilingi bilioni 300, sekta binafsi wanaweza kuja
kushirikiana na Serikali kwa kuanzisha viwanda vitakavyosaidia sekta hiyo ya
kilimo” alisema Rais Magufuli.
Kuhusu matumizi ya lugha ya kiswahili, Rais Magufuli alisema aliamua
kuzungumza kiswahili kwa sababu kiswahili ni utamaduni wa mtanzania, lakini ni
lugha ya kumi kwa kuwa na wazungumzaji wengi duniani, na ni lugha ya pili
Afrika.
Hivyo, amewataka watanzania kukithamini zaidi kiswahili, licha ya kuwa
wanaweza kujifunza lugha nyingine zozote.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli ambaye amezungumza baada ya kusikiliza
mada tano zilizotolewa na wanataaluma wakongwe wa uchumi, lugha, siasa na
utawala amnbapo Rais aliahidi kufanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa
katika kongamano hilo, ambayo anaamini yataleta tija na maendeleo kwa Taifa.
Mada zilizowasilishwa na kujadiliwa ziligusia masuala mbalimbali kama
vile viwanda, nishati ambapo ifikapo mwaka 2020 vyanzo vya nishati jadilifu na
visivyojadilifu vitazalisha megawati 5,000 na mwaka 2025 megawati 10,000
za umeme.
Aidha, mafanikio mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na ukuaji wa uchumi kwa
asilimia saba na jitihada sahihi zinazofanywa kuelekea asilimia nane, na
kufanya Tanzania kuongoza katika nchi za Afrika Mashariki, na kuwa
miongoni mwa nchi 5 za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.
Vile vile, katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya
Tano, pamoja na mafanikio mengine makubwa ya kufufua miradi ya msingi wezeshi,
kama ununuzi wa ndege saba, uboreshaji wa bandari, viwanja vya ndege na
barabara ni fursa ya kuwezesha miaradi mingine ya kiuchumi,mfano,viwanda vipya
zaidi ya 3,066, vilivyojengwa vitahitaji huduma za maji umeme, barabara,
bandari kama mahitaji wezeshi ya msingi.
Huduma kama usafiri wa anga zimeboreshwa, ikiwemo sekta ya utalii ambapo
mikakati ya sekta hiyo, matarajio yake mwaka ujao watalii wanaotarajiwa
kutembelea Tanzania wataongezeka hadi kufikia milioni 2, kiwango kitakachokuwa
karibu mara mbili ya watalii waliokuwa wanatembelea Tanzania miaka ya nyuma.
Katika kongamano hilo, wahudhuriaji walipata fursa ya kujadili mada
zilizotolewa, ambazo kwa ujumla tafiti za mada zimebaini juhudi kubwa
alizofikia Rais na Serikali yake kwa muda mfupi na wasomi tafiti zao zimebaini
kuwa miradi mikubwa inayoendelea vema, itawezesha miradi mingine
kuanzishwa au kufufuliwa na kuleta maendeleo, mfano ujenzi wa Umeme ni mradi
utakaowezesha ujenzi wa viwanda, pia wameeleza changamoto na kutoa maoni.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri,
makatibu wakuu na watendaji mbambali wa Serikali, wakiwemo viongozi
wastaafu, wabunge pamoja na wanafunzi wa vyuo na sekondari.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa
Mshiriki Maalum akiwa pamoja na washiriki wengine wakisikiliza mada mbalimbali
zilizokuwa zikitolewa na Watoa Mada katika Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa
katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano lililofanyika
katika ukumbi wa Nkuruma uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa
Mshiriki Maalum, akizungumza na Wageni mbalimbali wakiwemo Wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Viongozi wa Kiserikali, Mabalozi kutoka nchi
mbalimbali, pamoja na wananchi waliohudhuria katika Kongamano la
Hali ya Uchumi na Siasa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya
Tano lililofanyika katika ukumbi wa Nkuruma uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Baadhi
ya Washiriki wa Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa katika kipindi cha miaka
mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano wakisikiliza kwa makini wakati Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa
mshiriki Maalum alipokuwa akizungumza katika ukumbi wa Nkuruma katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment