Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya
ya Chalinze,Mheshimiwa Saidi Zikatimu akizungumza wakati wa kufungua ofisi ya serikali ya kijiji cha Tonga kilichopo kata ya Msoga.
.....................................
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, Mheshimiwa Saidi Zikatimu,amevitaka vijiji kutambua michango
mbalimbali ya wadau katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya
halmashauri ya Chalinze,agizo hilo amelitoa leo katika hafla ya ufunguzi wa
ofisi ya Serikali ya kijiji cha Tonga katika kata ya Msoga.
Ofisi ya serikali hiyo ya kijiji
imejengwa kwa ushirikiano wa halmashauri ya
wilaya,kijiji na wadau mbalimbali wa maendeleo katika halmashauri na kugharimu
jumla ya fedha za kitanzania milioni 25.1.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa
ofisi hiyo Zikatimu amewapongeza viongozi wa serikali ya kijiji cha Tonga kwa kuwatambua
wadau waliochangia katika ujenzi wa ofisi ya kijiji na kuwataka viongozi wa
vijiji vingine wilayani humo kuendelea kuwatambua na kuwashukuru kwa jitihada
wanazozifanya wadau katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Aidha Zikatimu katika hotuba yake ya
ufunguzi wa ofisi ya kijiji aliwataka vijana na wanawake kujiunga katika
vikundi na kupata mikopo kutoka mfuko wa vijana na wanawake unaotokana na
mapato ya halmashauri."Halmashauri tunazo pesa kwa ajili ya kuwakopesha
vijana bila riba tunatekeleza ilani kwa vitendo karibuni tuijenge nchi kwa
pamoja."
Aliendelea kuwashukuru wadau
mbalimbali wa maendeleo wanaojishughulisha na utatuzi wa kero mbalimbali kwa
kuipongeza kampuni ya SAYONA Fruits ambayo imekuwa ikiisaidia halmashauri ya
wilaya katika kuboresha huduma za jamii kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la
maabara na nyumba ya mganga katika kijiji cha Mboga.
Mwenyekiti wa halmashauri aliwataka
wananchi kuitumia ardhi na siyo kumiliki ardhi pasipo kuiendeleza na kwa
wanaomiliki ardhi bila kuiendeleza serikali itachukua hatua ikiwa ni pamoja
kuichukua ardhi hiyo na kuirejesha kwa wananchi ili itumike kwa mujibu wa
sheria taratibu na kanuni na si vinginevyo.
Hata hivyo Diwani wa kata hiyo
Hassani Mwinyikondo aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Tonga kwa kujitoa
kujenga ofisi nzuri na ya kisasa na hii ni namna ya kuboresha miundombinu
katika sekta ya utawala bora na kuvitaka vijiji vyote ndani ya kata ya Msoga
kuanzisha ujenzi wa ofisi za serikali za vijiji ili utoaji huduma kwa wananchi
uwe na tija.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, Mheshimiwa Saidi Zikatimu, akifungua ofisi ya serikali ya kijiji cha Tonga kilichopo kata ya Msoga.
No comments:
Post a Comment