Thursday, November 1, 2018

TIC -YAJIIMARISHA KUDHIBITI CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAWEKEZAJI

Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) akizungumza wakati alipotembelea banda la maonyesho ya ,kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) katika maonyesho ya bidhaa za viwandani Pichandege ,Kibaha Pwani.
 Picha na Mwamvua Mwinyi
..................................................


NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA

MENEJA wa kanda ya Mashariki wa kituo cha uwekezaji Tanzania( TIC ),Venance Mashiba ameeleza huduma za uwekezaji ni mtambuka ambapo zinatolewa na taasisi mbalimbali ambazo taratibu zake zikigongana inasababisha changamoto ya ucheleweshaji wa huduma kwa wawekezaji.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ,wakati wa maonyesho ya bidhaa za viwandani yanayoendelea Pichandege Kibaha ,mkoani Pwani , alisema tatizo lipo hasa katika upatikanaji wa ardhi na baadhi ya vibali vinavyochukua muda mrefu kwenye upatikanaji wake .

“Tatizo kubwa lipo kwenye ardhi kwani ardhi zote zipo chini ya halmashauri ,mwekezaji lazima apeleke wazo lake halmashauri na akipatiwa ardhi ndipo aje kwetu kuandikisha mradi wake “
“Sasa mradi wake utakubaliwa endapo atapata ardhi na taratibu za upatikanaji wa ardhi ni nyingi na ni ndefu”alifafanua Mashiba .

Mashiba alieleza ,kutokana na hilo kituo hicho , kimeimarisha huduma zake kwa kuongeza taasisi 11 za serikali ambazo zinatoa huduma mbalimbali, vibali na leseni ili mwekezaji apate huduma mahala pamoja na sio kuzunguka .

Alisema, ikitokea mwekezaji ana changamoto zinazohusiana na huduma zinazotolewa kwenye hizo taasisi basi wakuu wa taasisi hizo hukutana na kuamua kuzitatua .

” Tumeunda kamati maalum ya kitaifa inayojumuisha wakuu wa taasisi za serikali ambazo ni wadau katika kuhudumia uwekezaji ili kuharakisha utatuzi wa changamoto zinawakabili wawekezaji”alielezea Mashiba.

Nae mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo aliipongeza TIC kwa jitihada zake katika kukuza na kuvutia uwekezaji nchini na namna inavyohudumia wawekezaji kupitia huduma za mahala pamoja zinazotolewa na taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya ofisi za kituo hicho .

Alielezea kwamba ,Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayopokea wawekezaji na hivyo nguvu ya kuwahudumia iimarishwe. 
Ndikilo aliitaka TIC kuhakikisha inapata taarifa zinazohusiana na uwekezaji Mkoani humo kwa kuwasiliana na halmashauri za mkoa .

“Kwa kufanya hivyo kutarahisisha uratibu na huduma kwa wawekezaji wa Mkoa na Taifa kijumla ” alisema Ndikilo.

Ndikilo alisisitiza ni vyema wakawa na taarifa za maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa pamoja na ,takwimu za miradi ya uwekezaji.

Katika kuhakikisha mkoa wa Pwani unaendelea kuvutia wawekezaji Ndikilo alisema ,atawasilisha TIC maeneo ambayo tayari yametengwa kwa ajili hiyo ili yatafutiwe wawekezaji.

No comments:

Post a Comment