Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Lugoba, Alhaj
Abdallah Sakasa (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Saidi Zikatimu (kulia) siku ambayo shule hiyo ilipokea vifaa kutoka kwa wadau wa elimu.
.........................................................
Na Omary Mngindo, Lugoba Chalinze.
SHULE ya sekondari ya Lugoba iliyoko
Kijiji cha Lugoba, Kata Lugoba Halmashauri ya Chalinze, wilayani Bagamoyo
Pwani, inahitaji shilingi milioni 34 kuweka marumaru kwenye vyumba 17 vya
madarasa shuleni hapo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Alhaj
Abdallah Sakasa ameyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi
ofisini kwake, ambapo alisema kwa sasa madarasa 17 sakafu zake zimeharibika
kiasi cha kusababisha usumbufu kwa walimu pamoja na wanafunzi.
Alisema kuwa pamoja na kufanyiwa
ukarabati kwenye vyumba hivyo, lakini vimekuwa vikiharibika kutokana na
matumizi ya viti pamoja na meza zenye miguu ya vyuma hali inayochangia kutokea
kwa uharibifu wa sakafu hizo.
Alieleza kuwa kila chumba kimoja cha
darasa ili kuwekwa marumaru kinahitaji kiasi cha shilingi milioni mbili kwa
ajili ya ukarabati huo, hivyo kufanya kiasi vja sjilingi milioni 34 kujitajika
kwa kazi hiyo.
Aidha aliongeza kwa kuishukuru serikali
kutokana na juhudi zake za kuboresha elimu, sanjali na kuondoa ada na michango
mingine ambayo kwa kiasi fulani kilichangia baaadhi ya wazazi na walezi
kushindwa kuwasomesha watoto wao kutokana na michango hiyo.
"Kwaniaba ya walimu wenzangu,
tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Rais wetu Dkt. John Magufuli kwa kuelekeza
nguvu katika sekta ya elimu, sote tu mashahidi, amefuta ada na michango yote,
pia kutenga fedha kila mwezi zinazopelekwa kwenye shule," alisema Alhaj
Sakasa.
Alhaj Sakasa aliongeza kuwa shule hiyo
ilianzishwa mwaka 1989 kama shule za awali za wananchi, ina wanafunzi
wapatao 1,388 wanaendelea na masomo yao huku akitanabaisha kuwa kwa msimu wa
elimu kwa mwaka huu wanafunzi 173 wamemaliza elimu yao ya kidato cha nne.
Amewaomba wadau mbalimbali wajitokeze
katika kuhakikisha ukarabati huo unafanyika ili kuboresha ufundishaji shuleni
hapo.
No comments:
Post a Comment