Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula akifunga
mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili Wataalamu wa Mipango Miji jijini Dodoma.
....................................................
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mbaula
amewataka wataalamu wa mipango miji kuwa na mipango endelevu na kabambe
katika miji na halmashauri zote nchini ili kuwa na miji iliyopangika na kuepuka
ubomoaji nyumba za wananchi unaosababishwa na uelewa mdogo wa sheria na
taratibu za mipango miji.
Aliwataka wataalamu wa mipango miji kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza
majukumu yao kuepesha wananchi kuvunja sheria unaosababishwa na
wataalamu kutowaeleza ambapo alisema si kila mwananchi anayevunja sheria za
ujenzi mjini anafanya makusudi bali wengine hawajui sheria na taratibu na
kuhitaji kuelezwa.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili wa
Wataalamu wa Mipango Miji jijini Dodoma jana, Dk Mabula alesema maeneo
mengi ya miji wataalamu wanahangaika na kazi ya kurasimisha jambo ambalo siyo
suluhisho la upangaji miji bali ni kujaribu kuweka viraka katika vazi
lililochakavu.
Akigeukia suala la kuwepo maeneo mengi yasiyopangwa, kupimwa na
kumilikishwa Dk. Mabula alisema eneo hilo linaibua changamoto mbalimbali kwa
jamii ikiwemo ongezeko la makazi holela maeneo ya mijini, kukua kwa miji
isiyo na mpangilio mzuri pamoja na kukithiri kwa migogoro ya ardhi nchini na
kuwashauri wataalamu hao wa Mipango mijini nchini kuwafuata wananchi waliko kwa
ajili ya kutatua kero zao.
Alizitaka halmashauri ambazo muda wa mipango yake kabambe imeisha
kuhakikisha zinahuisha mipango hiyo ili kuwa endelevu kwa minajili ya
kuweka miji salama na ikiwa imeandaliwa miundo mbinu muhimu kwa mustakabali wa
maendeleo ya miji na taifa kwa ujumla.
Aidha, Dk. Mabula ametaka maeneo ambayo reli ya SGR inapita ni vyema
halmashauri za maeneo husika kuanza kufanya upangaji mapema ili reli
itakapoanza maeneo yote yawe yamepangwa, yamepimwa na yamemilikishwa na
uendelezaji umefanyika ili kuinua uchumi kwa maeneo husika na kutosubiri wajanja
wakaanza kuvamia.
Katika maazimio yake yaliyosomwa na Msajili wa Bodi ya Usajili wa
Wataalamu Mipango Miji Hellen Mtutwa, Washiriki walikubaliana Chuo Kikuu cha
Ardhi kwa kushirikiana na Bodi ya Usajili Wataalamu Mipango Miji kuandaa
muongozo utakaowawezesha Watendaji wa Kata na Vijiji kuwa wasimamizi wa mipango
miji kwenye maeneo yao ili kuepuka ujenzi holela na miji isiyopangwa.
Aidha, Washiriki walikubaliana urasimishaji wa makazi ufanayike katika
maeneo yote ya nchi na siyo baadhi ya maeneo na wataalamu mipango miji
kuhakikisha wanaandaa andiko la mradi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya upangaji miji badala ya kusubiri serikali pekee.
Mkutano huo wa Bodi ya Usajili Wataalamu Mipango Miji uliokuwa ukijadili
matatizo na changamoto zinazowakabili Wataalamu wa taaluma za Mipango Miji
katika shughuli zao na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo na
kushirikisha wataalamu 260 kutoka Serikali na Sekta Binafsi pamoja na Makampuni
yanayojishughulisha na mipango miji.
Sehemu
wa washiriki wa Mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji
uliofanyika jijini Dodoma. (Picha zote na Hassan Mabuye wa Wizara ya
Ardhi)
No comments:
Post a Comment