Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akikata utepe
kuzindua Ushirika wa Wavuvi Igombe jijini Mwanza, Kulia ni Mbunge wa Ilemela na
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula.
Kushoto ni Mwenyekiti wa ushirika huo, Paul Ngwegweu.
......................................
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amezindua Ushirika
wa Wavuvi katika Mwalo wa Igombe jijini Mwanza na kumuagiza Katibu Mkuu Uvuvi,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha ifikapo Disemba 31 mwaka huu kuwepo
na vyama imara vya ushirika visivyopungua 20 kwenye maeneo yote nchini ambako
shughuli za uvuvi zinafanyika ikiwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano
kuwainua wavuvi kutoka kwenye uvuvi wa kujikimu kwenda kwenye uwekezaji mkubwa
utakaowezesha kubadilisha maisha yao na kukuza uchumi wa nchi.
Hatua hiyo ya Serikali inakuja baada wavuvi kudharauliwa
kwa muda miaka mingi kutokana na shughuli wanayoifanya ambapo
taasisi za fedha ziliwadharau kwamba shughuli zao hazikopesheki na wala
hawawezi kupewa mikopo huku wachuuzi wa mazao ya uvuvi wakiwa ni matajiri
wakubwa lakini wale wanaoingia majini kuvua wameendelea kuwa masikini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Chama cha Ushirika wa
Wavuvi Igombe Limited Ilemela jijini Mwanza, Waziri Mpina amesema Serikali ya
awamu ya Rais Dk. John Pombe Magufuli imekataa wavuvi na shughuli za uvuvi
kudhauriwa tena ndio maana inatilia mkazo suala la ushirika na kuwaunganisha na
taasisi za kifedha na kuanza kukopeshwa.
Hivyo Waziri Mpina akasisitiza kuwa sasa Wavuvi wanatoka kwenye
kupuuzwa na kudhauliwa wanaingia kwenye kundi la kuheshimiwa na kupewa heshima
inayostahili kulingana na shughuli yao ambayo Taifa inaitegemea kukuza uchumi
na kuipatia nchi fedha za kigeni ambapo mauzo ya samaki nje ya nchi yamefikia
shilingi bilioni 691 kutoka sh bilioni 379 mwaka 2018 na kulifanya zao la
samaki kuongoza kwa kuipatia nchi fedha za kigeni.
Pia kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya
kukuza sekta ya uvuvi na kuwaendeleza wavuvi uagizaji wa samaki kutoka nje ya
nchi umeshuka kwa kiwango kikubwa kutoka wastani wa sh. Bilioni 56 mwaka
2017 hadi kufikia sh bilioni 17 mwaka 2019.
“Mwaka huu wa fedha hatutarajii kutumia hata senti moja ya
kununua samaki kutoka kwa sababu samaki hao sasa mnavua ninyi na soko lote
mnalihudumia hatuna sababu ya kuagiza tena samaki kutoka nje ya nchi, Sisi
Wizara na wavuvi wangu tunaishukuru sana Benki ya Posta kwa kuunga mkono
jitihada za wizara hii na jitihada za wavuvi na kazi kubwa wanayoifanya kwa
kuwafungulia akaunti maalumu bila masharti yoyote”alisema Mpina.
Waziri Mpina alisema ushirika huo wa Igombe kwa sasa una
mtaji wa shilingi milioni 20 ambazo zimetokana na mchango wa wanachama wenyewe
sh milioni 7.5, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi imewachangia sh.
milioni 10 na Mbunge wa Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula amechangia sh. milioni 2.5.
Waziri Mpina ameunga mkono mpango wa ushirika huo wa
kujenga kiwanda cha kutengeza barafu na kumuagiza Mratibu wa Dawati la Sekta ya
Binafsi Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutengeza mkakati wa haraka na kwamba ifikapo
Disemba 31 kiwanda cha barafu kizinduliwe rasmi ili uwe ushirika wa mfano wa
wavuvi Tanzania. Pia Mpina amemuomba Mbunge wa Ilemela, Mabula aweke jiwe la
msingi la kuanza ujenzi wa kiwanda hicho Novemba mwaka huu kwani na yeye
anamchango mkubwa katika kufanikisha uanzishwaji wa ushirika huo.
Waziri Mpina alisema sasa kuna jumla ya vyama 7 vya
ushirika wa wavuvi ambavyo ni Igombe Mwanza, Ikumbaitale Chato, Kigangama Magu,
Ihale Magu, Bukombe Fishing Corperative Society Sengerema, Zilangula Fishing
Cooperative Sengerema, Umamiki Fishing Cooperative Society Sengerema.
“Kampeni ya ushirika sio maagizo ya Mpina ni maagizo ya
Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 ibara ya 27 (a-b) ambayo
ilitaka Serikali kuhakikisha inaanzisha na kuimarisha vyama vya ushirika
“alisema Mpina.
Kuhusu mabadiliko ya sheria, Waziri Mpina alisema tayari
Serikali imeruhusu matumizi ya leseni moja ya uvuvi kila maji na kuondoa ukomo
sangara sentimita 85 sasa kuanzia sentimita 50 na kuendelea huku wavuvi
wakiruhusiwa kuvua kwa kutumia nyavu za kuanzia nchi sita na kuendelea
kwa Ziwa Victoria.
Katibu wa Ushirika wa Igombe, Dunia Isomba alisema
ushirika huo ulianza na wanachama 22 lakini sasa wamefikia 46 na walianza na
mtaji sh. Milioni 7.5 na baadae Wizara ya Mifugo na Uvuvi inawachangia milioni
10 na Mbunge Dk Mabula milioni 2.5 ambapo kwa sasa wanakusudia kuanzisha
kiwanda cha barafu, kununua gari la kubeba samaki kwenda viwandani na kuanzisha
duka la kuwa na zana za uvuvi zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria
na kuishukuru Serikali ya Rais Dk. Magufuli kwa namna ilivyojipambanua
kuwasaidia na kuwainua wavuvi.
Mbunge wa Ilemela, Dk. Mabula mbali na kuchangia milioni
2.5 pia ameahidi kuchangia tofali zitazowezesha kuanza ujenzi wa kiwanda cha
kutengeneza barafu cha ushirika huo.
No comments:
Post a Comment