TAMASHA la 38 la Sanaa Bagamoyo
linaanza rasmi kesho Oktoba 19-26 katika mji wa kihistoria Bagamoyo mkoani
Pwani.
Mwaka huu tamasha hilo litaanza kwa
mtindo wa tofauti na ilivyozoeleka, litaanza kwa kuzunguka mitaa mbalimbali ya
wilaya hiyo, lengo likiwa ni hamasa kwa tukio hilo muhimu.
Wasanii wa kazi mbalimbali
watazunguka mji huo kwa ngoma mbalimbali ili kuwachochea wadau kujitokeza
katika ukumbi ulioko chuoni hapo.
Zoezi hilo la kuzunguka maeneo ya
Bagamoyo, litaanza asubuhi likishirikisha wadau mbalimbali.
Bagamoyo ni mojawapo ya maeneo yenye
urithi na utajiri mkubwa wa kiutamaduni Ulimwenguni, ambako Tamasha hilo la
kimataifa, kwa mara nyingine tena litawakutanisha wasanii mbalimbali kutoka
ndani na nje ya nchi, ambao wataonesha kazi zao za sanaa na utamaduni.
Dk. Hebert Makoye, ni Mtendaji Mkuu
wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), ambao ni waandaaji wa
tamasha hilo linalozidi kujizolea umaarufu kila mwaka, anasema lengo ni
kuendeleza na kudumisha Utamaduni wa Mtanzania, kubadilishana uzoefu na
kujifunza kutoka kwa mataifa mengine kupitia warsha, kongamano na maonyesho
mbalimbali.
Dk. Makoye, anasema tamasha la 38
linatarajiwa kushirikisha wasanii zaidi ya 100 ya hapa nchini na nje, likiwa na
dhamira ya kubadilishana uzoefu katika sanaa, hivyo ni nafasi ya wadau
mbalimbali wa sanaa kujitokeza na kushuhudia elimu kutoka kwa wasanii
watakaopanda jukwaani.
Anasema, tamasha la mwaka huu
litashirikisha vijana wa shule za Msingi na Sekondari kutoka Bagamoyo, Vyuo na
Vyuo Vikuu.
“Mwaka huu, tamasha linatarajiwa
kuhudhuriwa na jumla ya watazamaji 60,000 kutoka maeneo ya Bagamoyo, Dar es
Salaam na sehemu zingine za Tanzania pamoja na nje ya nchi,” anasema Dk. Makoye
na kuongeza.
Kusudi la Tamasha hili ni kutoa fursa
kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi, pamoja na watazamaji kukutana na kuuenzi
utajiri wa utamaduni wao unaowatofautisha na mataifa mengine, ambao unaonyesha
utofauti wao katika muktadha wa maadili na mshikamano, pamoja na ubunifu.
Malengo maalum ya Tamasha
Dk. Makoye, anasema ni jukwaa kwa
wanafunzi wa TaSUBa na wa kutoka taasisi zingine za mafunzo, kuonesha kazi zao
na stadi walizopata katika mafunzo yao ya sanaa na utamaduni.
Anasema, pia ni kukuza na
kubadilishana tamaduni kati ya wasanii wa ndani na wa kimataifa, ni jukwaa la
wasanii wachanga kuonesha vipaji na ustadi wao kwenye sanaa na utamaduni,
kuongeza uhamasishaji miongoni mwa vijana na wasanii juu ya masuala yanayohusu
sanaa, michezo na utamaduni wa Kitanzania.
Dk. Makoye, anasema Kauli mbiu ya
Tamasha la mwaka huu ni ‘Sanaa na Utamaduni Ajira Yangu’.
Aidha, anasema katika tamasha la
mwaka huu, kutakuwa na maonesho ya bidhaa mbalimbali za sanaa na za
kiutamaduni, vyakula mbalimbali kama vile nyama choma, samaki, pamoja na
vyakula vya baharini.
Pia, anasema wageni watapata fursa ya
kutembelea mji wa kihistoria wa Bagamoyo.
TaSUBa, Clouds Plus kuboresha tamasha
Mapema mwaka huu, TaSUBa imeingia
makubaliano na Kampuni ya Clouds Plus Production yenye lengo la kushirikiana
katika kusaka rasilimali za uendeshaji wa Tamasha hilo la Kimataifa la 38.
Akizungumza wakati wa hafla ya
kusaini makubaliano iliyofanyika ukumbi mkubwa wa maonesho wa TaSUBa, Dk.
Makoye, anasema lengo kuu la makubaliano hayo ni kutafuta rasilimali
zitazowezesha kuendesha tamasha hilo lenye lengo la kuenzi, kudumisha na
kutunza utamaduni wa Mtanzania.
Anasema tangu kuanzishwa kwake mwaka
1982, tamasha limekuwa likifanyika kila mwaka bila kukosa mbali na kukumbwa na
uhaba wa fedha, lakini anaamini kwa kushirikiana na kampuni kubwa ya biashara
ya Clouds Plus Production, tamasha linaweza kuvutia wawekezaji mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Uendeshaji wa Clouds
Plus Production, Ramadhani Bukini, anasema kampuni yake inayomiliki runinga na
redio, itatumia mbinu mbalimbali kulitangaza tamasha hilo Duniani ili kufanya
lifikie malengo yake ya kuenzi na kudumisha utamaduni wa Mtanzania na
pia kuvutia wawekezaji wengi.
Ratiba mahsusi
Dk. Makoye, anasema katika wiki ya
tamasha zipo siku zitakuwa maalum kwa ajili ya ratiba mahsusi, ambako Jumatatu
itakuwa ni ‘Usiku wa Filamu’, Jumatano ‘Usiku wa Muziki wa Dansi’ na Jumapili
‘Usiku wa Taarabu’.
Wasanii wanaotarajiwa kupanda
jukwaani
Wasanii wanaotarajiwa kupanda
jukwaani mwaka huu ni Khamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, Juma Kassim ‘Juma Nature’,
Barnaba Elias ‘Barnaba’, Dullah Makabila, Gigy Money na Vitalis Maembe.
Wengine ni Mashauzi Classic, Malkia
Khadija Kopa, Thabit Abdul, Bendi ya Msondo Ngoma, John Kitime na bendi yake,
Sisi Tambala, Sinaubi Zawose, Shada Acrobatics na Baldreda kutoka Marekani.
Dk. Makoye, anabainisha kuwa pia
makundi ya hapa nchini yatashiriki, ambapo Bagamoyo itatoa 37, Dar es Salaam
28, Zanzibar mawili huku mikoa ya Mwanza, Ruvuma, Morogoro,
Kilimanjaro, Njombe yatatoa kundi moja moja, Arusha mawili na Dodoma 10.
Makundi kutoka nje ya Tanzania, Marekani
yatakuwa mawili, Botswana, Korea Kusini, Zimbabwe, Uganda, Zambia na Finland
kundi moja moja huku kutoka Kenya yakiwa nane.
Mgeni rasmi ufunguzi/ufungaji
Dk. Makoye, anaweka wazi mgeni rasmi
wakati wa ufunguzi katika tamasha la mwaka huu, anatarajiwa kuwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe huku wakati wa
kufunga atakuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juliana Shonza.
No comments:
Post a Comment